Kocha Bakari Shime Aipongeza TFF kwa Kuandaa Ligi ya Wasichana Shule za Msingi Dar es Salaam

Kocha wa timu za Taifa za wanawake Bakari Shime amesema kuwa TFF imefanya jambo la msingi na kubwa kwa kuandaa mashindano ya CAF ya ligi ya wasichana wa shule za msingi waliochini ya umri wa miaka 15; ligi ambayo inashirikisha timu nane kutoka maeneo tofauti tofauti ya Mkoa wa Dar es Salaam.

Kocha Shime aliyasema hayo asubuhi ya tarehe 15 Agosti, 2020 alipohudhuria kwenye mechi za uzinduzi wa ligi hiyo zilizofanyika katika viwanja vya Karume; yalipo makao makuu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Akielezea kuhusu programu hiyo, Bakari Shime alisema kuwa jambo lililofanywa na TFF lina tija kubwa na linapaswa kuungwa mkono na kuendelezwa na kwamba hiyo ni hatua muhimu sana katika kuendeleza mchezo wa soka la wasichana na vijananja Nchini.

Shime aliongeza kuwa kila kitu kinahitaji msingi, na ili nchi iweze kupata wachezaji wazuri na bora ni sharti ianze kuwekeza kuanzia ngazi ya chini kabisa kama TFF inavyofanya  sasa.

Kocha Shime aliendelea kufafanua zaidi kuhusu suala la kuwekeza mpira kwa watoto wadogo akidai kuwa ni njia na mbinu sahihi yenye kuweza kuleta manufaa zaidi kuliko kungojea mashindano ya UMITASHUMITA na UMISETA pekee ambayo hufanyika kwa msimu tu.

Aidha Kocha Shime alieleza kuvutiwa kwake na programu hiyo iliyomsababisha mpaka akamua kukaa yeye akiwa na baadhi ya wasaidizi wake akiwa pamoja na kocha msaidizi Edna Lema, wakifuatilia mashindano yeyote yanayohusisha timu za wanawake/wasichana.

Kocha Shime alieleza kwamba wamekuwa wakifanya hivyo kwa umakini wa hali ya juu ili waweze kubaini na kugundua vipaji vilivyopo katika timu tofauti tofauti Nchini huku lengo likiwa ni kutaka kujua maeneo   ambayo wachezaji  hao wanaweza kupatikana na wapi wanafaa kutumika katika timu za taifa.

Vile vile, wamekuwa wakifanya hivyo, ili basi nao waweze kupendekeza majina na kuyafikisha kwa mkurugenzi wa ufundi wa TFF kwa ajili ya kuyafanyia kazi zaidi.

Akihitimisha mazungumzo yake kocha Shime aliushukuru uongozi wa TFF uliopo sasa unaoongozwa na Rais Wallace Karia na Katibu Mkuu Kidao Wilfred pamoja na viongozi wengine kwa kukubali kuandaa mashindano hayo muhimu kwa maendeleo ya mpira wa miguu kwa wanawake na vijana wa Tanzania.