kocha Shime: “Haitakuwa mechi rahisi, Ila tumejipangaa kupata matokeo”

Kocha mkuu wa timu ya Taifa ya wanawake Twiga Stars Bakari Shime amesema  mchezo wa marudiano wa kufuzu Olimpiki dhidi ya Botswana hautakuwa mchezo rahisi lakini kikosi chake kimejipanga vizuri kuhakikisha kinapata matokeo mazuri ugenini na kuweza kusonga katika hatua inayofuata.

Hayo ameyasema alipokuwa akizungumza na wanahabari kuelekea katika mchezo huo utakaochezwa kesho Oktoba 31,2023  katika uwanja wa Taifa wa Botswana majira ya sa 12 kamili Jioni kwa saa za Afrika ya Kusini na saa 1 kamili usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

Kocha Shime alisema, Mchezo huo utakuwa mgumu kutoka na kwamba Botswana inafahamu vizuri namna ya uchezaji wa kikosi chake na mapungufu yake hivyo watayatumia mapungufu hayo kujaribu kupata matokeo. Lakini yote kwa yote nina imani kwamba kikosi kipo tayari kupambana na kurudi na ushindi nyumbani.

“Mbinu yetu kubwa katika mchezo wa kesho itakuwa ni kushambulia kwa muda wote wa mchezo na kuhakikisha tunamiliki mpira kwa muda mrefu ili kuwanyima wapinzani wetu nafasi ya kupata magoli. Kuhusu afya za wachezaji  wote wako salama isipokuwa nahodha Amina Bilali na beki wa Kati Anastazia katunzi ambao hawakua sehemu ya kikosi  katika mchezo wa awali lakini kwa sasa wanaendelea vizuri na inawezekana wakawa sehemu ya kikosi katika mchezo wa marudiano”  alisema Kocha Shime.

Mbali na mchezo Kati ya Botswana dhidi ya Tanzania, michezo mingine ya kufuzu  Olimpiki itakayochezwa Oktoba 31, 2023 ni Cameroon dhidi ya Uganda ambapo Uganda ilishinda goli 2-0 katika mchezo wa awali huku Morocco akienda kujiuliza mbele ya Namibia baada ya ushindi wa goli 2-0 katika mchezo wa awali uliochezwa Oktoba 26, 2023.