Kocha Shime: Mechi za kirafiki zinatuandaa kuelekea mashindano ya kimataifa

Kocha mkuu wa timu za taifa za wanawake Bakari Shime amesema mechi za kirafiki za kalenda ya FIFA zinawaandaa wachezaji kujiweka tayari kuelekea mashindano ya kimataifa.

Hayo ameyasema mara baada ya mchezo wa kirafiki Kati ya Algeria dhidi ya Tanzania kumalizika katika uwanja wa Nelson Mandela Baraki nchini Algeria ambapo Twiga Stars ilipoteza mchezo huo kwa goli 4-0.

“Ni mchezo ambao umetupa sura halisi ya namna timu yetu ilivyo kwasasa kutokana na kwamba Twiga stars haijakaa pamoja muda mrefu na hawakua na mashindano yoyote kwa zaidi ya miezi 6, hivyo ilikua ni sehemu nzuri ya kujitathimini na kuona tunaanzia wapi kujiandaa na mashindano yajayo” alisema kocha Shime

Kocha huyo aliongeza kuwa, kukosekana kwa baadhi ya wachezaji wa Twiga stars wanaocheza nje ya Tanzania ilipunguza nguvu ya kikosi hasa Katika eneo la ushambuliaji lakini ukiangalia kwa picha kubwa imekua ni faida kwa wachezaji waliopo kuonyesha viwango vyao kwa kucheza na timu kubwa ambayo imeshiriki AFCON mara tano na katika viwango vya FIFA iko nafasi ya 80 wakati Twiga Stars ikishika nafasi ya 152.

Ratiba ya michezo ya kirafiki ya kimataifa itaendelea tena leo Aprili 10,2023 ambapo Timu ya taifa ya wanawake chini ya umri wa miaka 20 (Tanzanite Queens) itacheza na timu ya taifa ya wanawake chini ya miaka 20 ya Algeria majira ya sa nne na nusu usiku kwa saa za Algeria lakini saa sita na nusu usiku kwa saa za Afrika Mashariki katika uwanja wa Nelson Mandela Baraki, Algeria.