Kocha Shime: Tumejifunza mengi, tutajipanga wakati mwingine

Kocha mkuu wa timu ya wanawake chini ya miaka 20 ‘Tanzanite Queens’ Bakari Shime amesema  licha ya kupoteza katika mchezo wa marudiano wa kufuzu kombe la Dunia dhidi ya Nigeria wamejifunza na wamepata uzoefu wa kutosha hivyo anakwenda kujipanga kwa mashindano yajayo.

Hayo ameyasema baada ya mchezo huo kumalizika katika uwanja wa Moshood Abiola, Nigeria ambapo Nigeria ilipata ushindi wa goli 2-1 na hivyo kutinga katika raundi ya nne kwa jumla ya magoli 3-1.

Kocha Shime alikipongeza kikosi chake kwa kucheza vizuri licha ya mapungufu madogo yaliyojitokeza ambayo yaliigharimu timu katika kipindi cha pili. Mbali na mapungufu hayo bado uwanja uliotumika kwa mchezo haukuwa rafiki kwa aina ya uchezaji wa kikosi chake.

“Tumepoteza mchezo  lakini hatujapoteza malengo, timu za wanawake bado zina  mashindano mengi ambayo tuna nafasi ya kufanya vizuri. Bado tupo kwenye mbio za kufuzu WAFCON pamoja na Olimpiki na kote huko nafasi ya kufuzu bado iko wazi”. Alisema  Shime.

Timu ya Nigeria itacheza na Burundi katika raundi ya nne na ya mwisho ya kufuzu kushiriki Fainali za kombe la Dunia kwa wanawake chini ya miaka 20  ambapo mshindi Kati ya timu hizo atakata tiketi ya moja kwa moja  kushiriki mashindano hayo yatakayofanyika nchini Columbia mwaka 2024.