Kocha Shime: wachezaji wako tayari kuikabili Nigeria

Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya wanawake chini ya miaka 20  ‘Tanzanite Queens’ Bakari Shime amesema  kikosi chake kipo tayari kuikabili timu ya Nigeria katika mchezo wa mkondo wa pili wa kufuzu Kombe la Dunia utakaochezwa Novemba 19, 2023.

Hayo ameyazungumza mara baada ya mazoezi  ya kwanza kumalizika katika uwanja wa Turf Arena, Nigeria.

Kocha Shime alisema,  timu imepata nafasi ya kufanya mazoezi yake ya kwanza mara baada ya kuwasili nchini Nigeria ambapo wachezaji wameonyesha utayari na morali yao iko juu hivyo anaamini  kwamba matokeo mazuri yatapatikana.

” Hii ni mechi ya muhimu sana kwetu na tunaichukulia kwa ukubwa huo kwasababu kila timu ina nafasi sawa ya kusonga mbele katika hatua inayofuata.Tumefanya maandalizi ya kutosha toka tukiwa nyumbani Tanzania ambayo tunaamini yatatupa ushindi katika mchezo wa marudiano tukiwa ugenini.” Alisema Kocha Shime.

Mchezo wa mkondo wa pili kati ya Nigeria dhidi ya Tanzania utachezwa Jumapili Novemba 19,2023 katika uwanja wa Taifa (Moshood Abiola) uliopo Abuja, Nigeria majira ya saa 10 kamili Jioni kwa saa za Afrika Magharibi na saa 12 kamili Jioni kwa saa za Afrika Mashariki.