Mkatusaidie Kuzalisha Vijana Wengi Zaidi Kwenye Mpira
Agizo hilo limetolewa Januari 04, 2022 na Makamu wa Kwanza wa Rais TFF Athumani Nyamlani alipokuwa akiwakabidhi vyeti washiriki wapatao 51 waliohitimu kozi ya CAF D Diploma iliyo fanyika makao makuu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania.
“Nimefurahi tunafanya uzalishaji wa makocha wengi nchini kwani hilo ndilo hasa lengo letu TFF katika kufikia maendeleo ya mpira wa miguu hivyo naamini mtaenda kutusaidia kuzalisha vijana wengi zaidi ili tuwe na uwanja mpana wa kufanya machaguo ya wachezaji vijana wenye vipaji, uwezo na nidhamu”. Yamesemwa na Makamu wa Kwanza wa Rais TFF.
Aidha alisema kuwa mpira wa miguu unatakiwa uendeshwe kisayansi kama ambavyo Shirikisho limekuwa kilifanya hivyo kwa kuandaa na kuendesha kozi mbalimbali za Utawala, Ukocha na maeneo mengine katika tasnia hiyo ya mpira wa miguu.
Akizungumza Mkurugenzi wa Ufundi TFF Oscar Mirambo ambaye pia ndio alikuwa mkufunzi wa hiyo kozi alisema kuwa hana wasiwasi na washiriki hao kutokana na mabadiliko aliyoyabaini kutoka kwao kwa kipindi chote hicho cha kozi.
Alielezea pia kuhusiana na nafasi ya upendeleo ambayo wamewapatia wahitimu hao kuweza kuendelea na hatua inayofuata ya CAF C Diploma muda mfupi tu mara baada ya kuhitimu kwenye hatua hiyo licha ya utaratibu uliozoeleka kuwa kila mshiriki anapaswa kufanyia kazi mafunzo yake kwa muda wa mwaka mmoja kabla ya kuendelea na ngazi za juu zaidi za mafunzo hayo ya ukocha.
Hata hivyo licha ya kozi hiyo kusheheni washiriki wanaume, alikuwepo pia mwanamke mmoja Rehema Chuka ambaye aliweka wazi matamanio yake ya kushiriki kozi nyingi zaidi ili kuwa ni mfano mzuri kwa wanawake wengine, Aidha aliwashukuru TFF kwa kuandaa na kuendesha mafunzo hayo.
Naye Henry Hezron Mwaluseke ambaye pia ni mshiriki wa kozi hiyo akizungumza kwa niaba ya washiriki wengine alisema “Sisi ni kati ya walimu ambao ni zao la TFF, tulikuja kuongeza ujuzi na tayari tumeupata hivyo tunaahidi kuwa mabalozi wazuri na wakubwa kwenye mlilolianzisha TFF”.
Washiriki wa kozi hiyo ni; Peter .R. Salvatory, Martin .L. Zephania, Ernest .W. Lusulo, Henry .H. Mwaluseke, Stavanger .P. Nyambasi, Rehema .R. Chuka, Gervas .M. Kamali, Bukulu .J. Kakopa, Awadhi .M. Kilaya, Augustino .A. Mjomba, Mohamedi .B. Kolumba, Peter .S. Shundah, Khalifa .O. Idrissa, Isaya .A. Mganda.
Na wengine ni; Moses .A. Kasembe, Adelard .P. Mishinga, Benedictor .O. Ndira, Hussein .A. Muhammed, Hassan .A. Kambi, Dotto .J. Rufili, Ibrahim .A. Dizele, Goodluck .E. Ngonyani, Khalifa .R. Mfate, Bakari .J. Juma, Twail .T. Ndyanabo, Salum .N. Amour, Abinery .M. Chitungo, Abdulkarim .M. Abdulkarim, Athumani Rahim, Hilali .U. Magenge na Ashrafu .S. Kattendah.