Kozi ya Diploma ‘A’ CAF Yaanza TFF

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupitia Idara yake ya Ufundi limeendelea kutoa Kozi ya Stashahada ‘A’ ya CAF kuanzia Agosti 02, 2021 katika darasa linaloendeshwa kwenye Makao Makuu ya Shirikisho hilo yaliopo Karume-Ilala-Dar es Salaam.

Kozi hiyo inayojumusha washiriki kumi na nane (18) ni miongoni mwa kozi za daraja la juu katika taaluma za ukocha ambayo kwa kawaidi huhitaji washiriki wasiozidi ishirini kwa darasa moja na hutolewa kwa washiriki ambao tayari wanatimu wanazozifundisha na sio kwa kila muhitaji wa kozi.

Akizungumzia kuhusu utaratibu wa kozi hiyo, Mkurugenzi wa ufundi Oscar Mirambo alisema kuwa kozi hiyo itatolewa kwa muda wa mwaka mmoja ambapo muda huo utagawanywa kwenye vipindi vitatu. Kipindi cha kwanza huchukua siku kumi za masomo ya darasani na baada ya mafunzo ya nadharia washiriki hupewa muda wa kwenda kujifundisha kwa vitendo kwenye timu watokazo.

Mkurugenzi huyo aliongeza kufafanua kuwa utaratibu wa kutoa muda wa mafunzo kwa vitendo hufanyika kwa lengo la kutoa nafasi kwa washiriki hao kuonesha uelewa walioupata kwa kuwa kozi ya ukocha imejikita zaidi katika vitendo. Hata hivyo, washiriki hao hufuatiliwa kwa karibu zaidi pindi wawapo kwenye klabu zao ili kuweza kuwafanyia tathimini endapo wanazingatia yale walioelekezwa kwa nadharia.

Aidha, Mkurugenzi Mirambo alieleza kuwa kozi hiyo inafundishwa na wakufunzi wa CAF na FIFA pia huku akimtaja Kim Poulsen ambaye ni kocha Mkuu wa Taifa Stars kuwa ni moja ya wakufunzi hao ambao wanauzoefu wa kutosha katika tasnia hiyo ya ukocha pamoja na ukufunzi.

Mmoja kati ya washiriki wa kozi hiyo Edna Lema ambaye ni miongoni mwa makocha wanawake wanaowakilisha vizuri katika kazi hiyo ya kufundisha mpira wa miguu nchini, alisema kuwa yeye amejiunga na kozi hiyo kwa dhumuni la kuongeza elimu zaidi ili aweze fikia malengo yanayoambatana na ndoto zake za kuwa kocha mkubwa ndani na nje ya nchi hapo siku za usoni.

Kocha Edna aliongeza kuwa yeye anapenda kujifundisha vitu vipya ambavyo anaamini kuwa siku moja vitakuja kumlipa licha ya changamoto mbalimbali anazokutana nazo katika kazi yake.

Washiriki waliohudhuria kwa ajili ya kupata mafunzo hayo ya ukocha ngazi ya Stashahada  ‘A’ ya CAF ni; Mussa Omary, James Wambura, Muhbu Kanu, Patrick Okunu,  Edna Lema,Luhaga Makunja, Bakari Shime, Chisi Mbewe,Maalim Mohammed,Fulgence Mato, Alex Namazaba, Mohammed Muya, Khalid Muwisson, SAlvatory Augustino, Fikir Elias, Ngawina Ngawina na Denis Katambi.