Ligi Kuu ya NBC Yazidi Kusonga Huku Chungu Tamu Zikitawala

Ligi Kuu ya Tanzania Bara ilieendelea Novemba 26, 2022 kwa michezo mitatu kupigwa kwenye viwanja tofauti tofauti ambapo timu ya Namungo ikiiburuza timu ya Dodoma Jiji bao moja kwa sifuri, Singida Big Stars wakailaza Ruvushooting bao moja bila huku Young Africans nao wakiishushia kipigo cha mabao 2-0 timu ya Mbeya City.

Mchezo kati ya Namungo na Dodoma Jiji ulipigwa saa 08:00 mchana katika uwanja wa Liti Singida unaotumiwa na Dodoma Jiji kama uwanja wa nyumbani, wakati Ruvushooting wao wakitumia uwanja wa Uhuru, mchezo huo ukipigwa majira ya saa 10:00 jioni, ambapo Ruvu walishindwa kutamba mbele ya SBS huku mchezo wa tatu, kati ya Young Africans na Mbeya City ukichezwa majira ya saa 12:15 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam.

Wafungaji wa magoli katika michezo hiyo walikuwa ni Abdulmaliki Hamza kwa Namungo (dakika ya 82); wakati Frank Zacharia wa Singida Big Stars akiifungia timu yake goli kunako dakika ya 79 huku Fiston Mayele naye akizidi kuwaacha wafungaji wenzake kwa idadi ya magoli mara baada ya kupachika mabao 2 kwenye mchezo huo. Mayele aliandika bao la kwanza mnamo dakika ya 24 kipindi cha kwanza na dakika ya 79 kipindi cha pili akarejea tena.

Matokeo ya michezo hiyo ya Novemba 26, 2022 yamekuwa na faraja kwa baadhi ya timu huku yakipeleka hudhuni kwa timu nyingine. Timu ya Ruvushooting imejikuta ikiwa katika wakati mgumu zaidi baada ya kucheza mechi takribani 9 ikiambulia kipigo na sare, halikadhalika timu ya Dodoma Jiji ambayo nayo imeshindwa kuwa na muendelezo mzuri kwa kupoteza michezo kadhaa ikiwa nyumbani na ugenini pia, huku Mbeya City nao wakisuasua katika michezo yao mitatu ya hivi karibuni.

Kwa upande wa Singida Big Stars wao wamefanikiwa kuvuna alama 7 kwenye michezo mitatu, Namungo nao wakivuna alama sita kwenye michezo 6 huku Young Africans wao wakiendeleza kutokufunga na timu yeyote katika mechi 49 za Ligi Kuu Bara.

Baada ya michezo hiyo ya Novemba 26, timu ya Young Africans inasalia kileleni mwa Ligi ya NBC ikiwa na alama 32 ikishuka dimbani mara 12, Singida Big Stars inang’ang’ania nafasi ya nne ikiwa na alama zake 24 baada ya kucheza mechi 12 huku Namungo nayo ikiwa katika nafasi ya 8 baada ya kucheza michezo 13 ikikusanya alama 18.

Mbeya City naye yupo nafasi ya 7, akiwa na alama 19 baada kucheza mechi 13 wakati Ruvushooting wao wakishika nafasi ya 13 wakiwa wamecheza mechi 14 huku Dodoma Jiji wenyewe wakiwa katika nafasi yao ya 15 akiwa na alama 9 baada ya kushuka dimbani mara 13.