Ligi kuu ya U-20 kuendelea leo Azam Complex

Ligi kuu ya vijana chini ya umri wa miaka 20 (U-20) kuendelea leo katika uwanja wa Azam Complex Chamazi baada ya pazia kufunguliwa rasmi jana Julai 5, 2022 kwa michezo minne ya kundi A na C kupigwa, ambapo mchezo wa kwanza ulianza majira ya saa 8:00 mchana.

Mchezo huo wa mapema uliwakutanisha Biashara United dhidi ya Namungo na mpaka dakika 90 zinatamatika hakuna timu yoyote iliyoona lango la mwenzake. Mchezo wa pili ulipigwa majira ya saa 10:15 jioni uliwakutanisha Simba Sc dhidi ya Polisi Tanzania na Simba ilifanikiwa kuibuka kidedea kwa ushindi wa goli 2-1.

Baada ya mchezo huo wa pili kulipigwa michezo mingine miwili ambapo Tanzania Prisons walikutana na Wagosi wa Kaya (Coastal Union) ya Tanga. Mchezo huo ulianza majira ya saa 12:00 jioni na Tanzania Prisons ndiyo waliofanikiwa kuibuka na alama 3 kwa kuichapa bao 1-0.

Kutamatika kwa mchezo huo kati ya Coastal Union na Tanzania Prisons kulitoa nafasi kwa mwenyeji Azam FC kumkaribisha Mbeya City kutoka Mbeya. Katika mchezo huo Azam FC walitakata kwa kuichapa Mbeya City jumla ya mabao 3-2.

Muendelezo wa michezo ya ligi kuu ya vijana U-20 itaendelea tena leo kwa michezo minne ya kundi B na D kupigwa ambapo Mbeya Kwanza atamkaribisha  Ruvu Shooting majira ya saa 8:00 mchana huku Mtibwa Sugar akijiuliza kwa  Dodoma Jiji, KMC dhidi ya Kagera Sugar na mchezo wa mwisho utakuwa kati ya Young Africans  dhidi ya Geita  Gold Fc.