Pazia la Ligi Kuu ya Wanawake ya Serengeti Premium Lite limefungwa leo huku JKT Queens wakiibuka mabingwa bila kupoteza mchezo wowote.
Huu ni msimu wa pili mfululizo kwa JKT Queens kuchukua ubingwa bila kupoteza mchezo.
Katika mchezo wake wa leo JKT Queens imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Panama ya Iringa.
Mabao ya mabingwa hao yamewekwa wavuni na Asha Rashid na Zena Khamis.
Matokeo hayo yameifanya JKT Queens kujikusanyia alama 66 katika michezo 22 iliyoshuka dimbani.
Mechi nyingine zilizochezwa leo Alliance ya Mwanza imejihakikishia nafasi ya pili baada ya kupata ushindi wa mabao 17-0 dhidi ya Mapinduzi Queens na kufikisha alama 47 sawa na Simba ambayo imemfunga Marsh Queens ya Mwanza kwa mabao 6-0 mchezo uliochezwa Uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza.
Simba na Alliance wote wana alama 47 wakitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa Alliance akiwa na uwiano mzuri zaidi.
Mlandizi Queens imekamata nafasi ya nne kwa alama 43 baada ya kutoka suluhu 0-0 na Yanga Princess wakati Panama ya Iringa licha ya kufungwa mabao 2-1 na mabingwa JKT Queens wanakamata nafasi ya tano wakiwa na alama 42.
Evergreen ya Temeke Dar es Salaam iliyofungwa 4-2 na Kigoma Sister imeshuka daraja ikiungana na Mapinduzi Queens ya Njombe.
Mchezo mwingine Baobab Queens ya Dodoma na Tanzanite ya Arusha zimemaliza mchezo wao bila kufungana.
Ligi Kuu ya Wanawake ya Serengeti Premium Lite inadhaminiwa na bia ya Serengeti Lite.