Ligi ya Tff Wanawake Mkoa wa Dar es Salaam Yashika Kasi Raundi ya Tatu

Michezo ya raundi ya tatu Ligi ya Tff Wanawake mkoa wa Dar es Salaam imeendelea kupigwa kwenye viwanja vya Karume Ilala mwishoni mwa wiki hii kati ya tarehe 17,18 na 19 Machi, 2023 huku timu zote zikionekana kuimarika zaidi kiushindani.

Mchezo wa awali kupigwa kwenye duru hiyo ni ule uliowatoa kifua mbele The Eleven star Queens mpaka kwenye nafasi za juu ikifikisha jumla ya alama sita baada ya ushindi wa 2-1dhidi ya Tanzanite Princess iliyopoteza kwa mara ya tatu mfululizo.

Wakati The Eleven star wenyewe wakijipambanua kwenye msimamo wa ligi kwa ushindi huo, kule kileleni yuko Mbagala Queens anaezidi kuonesha makali yake kwenye ligi akifikisha alama 9 baada ya ushindi alioupata kwenye raundi zote tatu. Mchezo wa Machi 18, 2023 Mbagala Queens wenyewe walimpatia manyanyaso ukonga Queens kwa magoli 6-1.

Mbagala imezidi kuonyesha ubora wake kwenye ligi huku kocha mkuu Chande Mukil akisema kuwa wenyewe wamejitofautisha na wenzao kwenye mambo mwengi kwani hata mazoezi wenyewe huwa wanafanya kwa wiki nzima tofauti na wenzao ambao wanafanya kwa siku tatu au nne.

” Sisi tunafanya mazoezi kwa muda mrefu katika wiki, pia tunatumia uwanja mkubwa na wenye michanga ambao tunaamini unawajenga zaidi wachezaji wetu kumudu michezo ya viwanja vya nyasi” alisema kocha Mukil, sambamba na kutuma salamu kuwa lengo lao hasa ni kushiriki Ligi ya Mabingwa wa Mikoa.

Hata hivyo vita bado ni kubwa kwenye michuano hiyo ambayo kila raundi timu zinaonyesha kuimarika zaidi na huku zikivutana kugombea nafasi kwenye msimamo wa ligi, matokeo ya mechi nyingine za raundi ya tatu ni;Wisdom Queens 1-1 Kinondoni Queens, Young Star Queens 2-1 Sayari Women, Evergreen Queens 1-1 Temeke Sisters.

Mchezo wa kukamilisha raundi ya tatu utapigwa kati ya Ubungo Tafseo Queens na Mabibo Queens Machi 20, 2023 majira ya saa 2:00 asubuhi kwenye uwanja wa Karume Ilala.