Ligi ya Vijana U17 Yaendelea Kurindima Karume Dar.

Michezo ya Ligi ya Mkoa wa Dar es Salaam kwa wavulana umri chini ya miaka 17(U17) imeendelea kutimua vumbi kwenye uwanja wa Karume uliopo Makao Makuu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) leo Juni 25, 2022 kwa michezo miwili ya mapema kupigwa ambapo mchezo wa kwanza matokeo yalikuwa 3-1 huku ule wa pili ukiisha kwa matokeo ya 1-1.

Mchezo wa awali wa mzunguko wa tano  uliwakutanisha Green Worriors dhidi ya Cambiaso mnamo majira ya saa 2:00 asubuhi ambapo timu ya Cambiaso waliibuka washindi baada ya kuwaadhibu vijana wa jeshi kwa mabao 3-1.

Green Worriors ndiyo walikuwa wa kwanza kuandika bao la kuongoza mnamo dakika ya 10 ya mchezo huo, bao hilo lilifungwa na mchezaji jezi namba (20) aitwae Akido Venance lilidumu mpaka timu hizo zinakwenda kwenye mapumziko.

Dakika za mwanzo za kipindi cha pili Vijana wa Cambiaso walizinduka na kufanya ‘come back’ kwa kusawazisha bao mnamo (dkk 61); bao hilo likifungwa na mshambuliaji jezi namba 9 Sulemani Solomoni kabla ya Hussein Abdul kushindilia msumari wa pili kunako (dkk 67) na baadaye Sulemani akirejea tena langoni kwa vijana kutoka jeshini kwa kukomela msumari wa tatu na wa mwisho mnamo dakika ya 85 na kuufanya mchezo huo kukamilika kwa 3-1.

Mchezo wa pili ulizikutanisha Ruvu Shooting na African Sports, michi hiyo ikipigwa katika uwanja wa Karume pia; matokeo ya mchezo huo yalikuwa ni sare ya bao1-1. African Sports ndiyo waliotangulia kuandika bao mnamo dakika ya 20 kipindi cha kwanza kabla vijana wa Ruvu Shooting kusawazisha dakika ya 63 kipindi cha pili; matokeo yaliyodumu kwa dakika 90.

Michezo mingine ya ligi hiyo ya vijana wa U17, ya mzunguko wa tano itaendelea mchana wa leo  Juni 25, 2022 ambapo Vijana wa Azam FC watakuwa mwenyeji wa KMC majira ya saa 8:00 mchana; huku mechi ya mwisho ikiwakutanisha JKT dhidi ya Young Africans majira ya saa 10:00 na kuhitimisha mechi za Juni 25,2022.