Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Oktoba 5, 2018 ilipitia taarifa na matukio katika mechi za Ligi Kuu ya Tanzania (TPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) zinazoendelea hivi sasa.

Pia Kamati ilipitia malalamiko mbalimbali yaliyowasilishwa mbele yake na kufanya uamuzi ufuatao kwa upande wa TPL;

Mechi namba 24 (Coastal Union SC 0 vs KMC FC 0). Washabiki wa Coastal Union waliingia eneo la kuchezea (pitch) mara baada ya mchezo huo uliofanyika Septemba 1, 2018 kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga kumalizika huku waamuzi na wachezaji wakiwa bado hawajatoka, kitendo ambacho ni hatari kiusalama.

Kamati imeamua kuwa Coastal Union itakuwa kwenye kipindi cha uangalizi kwa mechi mbili zijazo, na iwapo washabiki wataendelea kuingia ndani ya uzio, timu hiyo itafungiwa kuutumia uwanja huo.

Mechi namba 33 (Ndanda SC 0 vs Simba 0). Timu ya Simba imepewa Onyo Kali kwa kutowasilisha orodha ya wachezaji wake (team match list) katika kikao cha maandalizi ya mechi. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Pia mchezaji Erasto Nyoni wa Simba SC anapelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kumpiga kiwiko Hassan Nassoro Maulid wa Ndanda SC, tukio hilo halikuonwa na Mwamuzi wa mechi hiyo iliyofanyika Septemba 15, 2018 katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

Mechi namba 34 (Tanzania Prisons 2 vs Ruvu Shooting 2). Timu ya Ruvu Shooting imepewa Onyo Kali kwa kutowasilisha orodha ya wachezaji wake (team match list) katika kikao cha maandalizi ya mechi hiyo iliyochezwa Septemba 15, 2018 kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Mechi namba 41 (Lipuli FC 1 vs Alliance FC 0). Pia Mwamuzi Msaidizi wa mechi hiyo Idd Mikongoti wa Dar es Salaam amefungiwa miezi sita kwa kushindwa kutafsiri sheria ya kuotea (off side), hivyo kukataa bao lililofungwa na Alliance FC. Adhabu dhidi yake ni kwa mujibu wa Kanuni ya 39(1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Waamuzi.

Mechi hiyo ilifanyika Septemba 19, 2018 kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora mjini Iringa.

Mechi namba 42 (Mbeya City FC 4 vs Ruvu Shooting 2). Mchezaji Ayoub Kitala wa Ruvu Shooting amefungiwa mechi tatu na faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumpiga kiwiko mchezaji wa timu pinzani.

Adhabu hiyo katika mechi hiyo iliyochezwa Septemba 19, 2018 Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 38(9) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Wachezaji.

Mechi namba 48 (Mbao FC 1 vs Simba 0). Klabu ya Simba imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na washabiki wake kuwarushia chupa za maji na soda viongozi, wachezaji na Kocha Mkuu wa timu yao baada ya mechi hiyo iliyochezwa Septemba 20, 2018 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kumalizika.

Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 43(1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Klabu.

Mechi namba 52 (Mwadui FC 1 vs Simba 3). Nahodha John Bocco wa Simba amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumpiga mchezaji wa timu pinzani.

Adhabu hiyo katika mechi hiyo iliyochezwa Septemba 23, 2018 Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 38(9) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Wachezaji.

Mechi namba 62 (Singida United 3 vs Mbeya City FC 0). Klabu ya Singida United imepewa Onyo Kali baada ya timu yake kuchelewa kwa dakika nane kwenye kikao cha maandalizi (pre match meeting) kwa ajili ya mechi hiyo iliyofanyika Septemba 26, 2018 Uwanja wa Namfua mjini Singida. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Mechi namba 65 (Azam FC 0 vs Lipuli 0). Meneja wa Azam FC, Simion Alando anapelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kosa la kumzonga Mwamuzi wa Akiba akilalamikia maamuzi ya Mwamuzi katika mechi hiyo iliyochezwa Septemba 27, 2018 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Mechi namba 72 (Simba SC 0 vs Yanga SC 0). Mchezaji James Kotei wa Simba anapelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kumpiga ngumi Gadiel Gabriel wa Yanga katika dakika ya 33, tukio ambalo Mwamuzi hakuliona katika mechi hiyo iliyofanyika Septemba 30, 2018 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Naye Andrew Vincent wa Yanga anapelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kumpiga kichwa Mohamed Hussein wa Simba katika dakika ya 61, tukio ambalo halikuonwa na Mwamuzi.

Mechi namba 76 (Ruvu Shooting 1 vs Mbao 0). Mwamuzi Fikiri Yusuf Saleh amepewa onyo kwa kushindwa kufanya maamuzi sahihi katika baadhi ya matukio yaliyojitokeza katika mechi hiyo iliyochezwa Oktoba 1, 2018 kwenye Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani.

Naye Kocha Msaidizi wa Mbao FC, Augustino Joseph Malindi anapelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kumfuata Mwamuzi na kumsakama kwa maneno na kumtolea vitisho vya kumroga.

LIGI DARAJA LA KWANZA
Mechi namba 1 (Ashanti United 1 vs Kiluvya United 1). Timu zote zimepewa Onyo Kali kwa kutowasilisha orodha ya wachezaji wake (team match list) katika kikao cha maandalizi ya mechi hiyo iliyochezwa Septemba 29, 2018 kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo.

Mechi namba 2 (Mashujaa 0 vs Polisi Tanzania 2). Timu ya Mashujaa imepewa Onyo Kali kwa kuchelewa kufika uwanjani kwa dakika 9 katika mechi hiyo iliyochezwa Septemba 29, 2018 kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo.

MALALAMIKO
Mwamuzi Athuman Lazi
Kamati imemuondolea adhabu ya kufungiwa miezi mitatu Mwamuzi Athuman Lazi baada ya kukubaliana na malalamiko yake kuwa jukumu la kuangalia off side katika mechi ni la Mwamuzi Msaidizi.

Mwamuzi Lazi alilalamikia uamuzi wa Kamati kumfungia miezi mitatu baada ya Mwamuzi Msaidizi Nicholas Makaranga kunyoosha kibendera kukataa bao la Ruvu Shooting dhidi ya KMC kuwa mfungaji aliotea wakati hakuwa ameotea.

Makaranga alifungiwa miezi sita kutokana na kitendo hicho katika mechi hiyo iliyofanyika Agosti 26, 2018 Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani na timu hizo kutoka sare ya bao 1-1.