Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) katika kikao chake Februari 9, 2019 chini ya Mwenyekiti wake Wakili Kiomoni Kibamba ilipitia mashauri 15 yaliyowasilishwa mbele yake na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania, na kufanya uamuzi ufuatao;

Mmiliki wa Changanyikeni Rangers FC, Omary Bawazir amepewa Onyo Kali kwa mujibu wa Ibara ya 10(a) ya Kanuni za Nidhamu za TFF baada ya kukiri kuingia uwanjani katika eneo la kuchezea (pitch) wakati wa mechi dhidi ya Cosmopolitan iliyochezwa Februari 2, 2019 Uwanja wa Chuo cha Bandari, Dar es Salaam.

Hata hivyo, Kamati imeshindwa kumtia hatiani kwa kosa la kumpiga Mwamuzi kutokana na Mlalamikaji kushindwa kuthibitisha tukio hio.

Pia Kamati imekazia faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa Changanyikeni Rangers FC iliyotolewa na Kamati ya Uendeshaji wa Ligi (Kamati ya Saa 72), na kuwa faini hiyo ilipwe ndani ya siku 30.

Katibu Mkuu wa Rhino Rangers, Bw. Dickson Mgalike amefungiwa miezi mitatu na faini ya sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kwa mujibu wa Kanuni ya 29(9) ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwa kuongoza washabiki wa timu yake kuwapiga waamuzi na kamishna baada ya mchezo dhidi ya Arusha United uliofanyika Februari 2, 2019 Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

Pia klabu ya Rhino Rangers imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na vurugu hizo. Faini inatakiwa kulipwa ndani ya siku 30 kwa kuzingatia Ibara ya 15(3) ya Kanuni za Nidhamu za TFF.

Mtunza Vifaa (Kit Man) wa Ruvu Shooting, Bw. Augustine Palangwa amepewa Onyo kwa kosa la kuzungumza na mwamuzi bila utaratibu katika mechi dhidi ya Yanga iliyofanyika Desemba 16, 2018 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Ibara ya 10(a) ya Kanuni za Nidhamu za TFF.

Kwa kosa la kutoa lugha ya matusi dhidi ya mwamuzi, Kamati haikumpata na hatia kwa sababu baada ya kupitia maelezo ya mlalamikaji na ripoti zote, kosa hilo limeshindwa kuthibitishwa kwa sababu ripoti za kamishna na mwamuzi zimetofautiana kuhusu tukio hilo.

Kamati imeridhia ombi la Yanga la kuahirisha kusikiliza shauri dhidi ya Abdallah Shaibu kwa vile wakati anapata mwito wa kuhudhuria akiwa mkoani.

Sasa shauri dhidi yake litasikilizwa katika kikao kijacho, na Kamati haitapokea udhuru wowote isipokuwa kama atakuwa na majukumu katika timu ya Taifa.

Bodi ya Ligi imemlalamikia mchezaji huyo kwa kumpiga kiwiko mchezaji wa Coastal Union katika mechi iliyozikutanisha timu Februari 3, 2019 kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Kiongozi wa Arusha FC, Hassan Issa amepewa Onyo na kutozwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) baada ya kutiwa hatiani kwa kutaka kumpiga Mwamuzi katika mechi ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) dhidi ya Arusha United SC iliyofanyika Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha.

Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Ibara za 10(a) na 15(2) za Kanuni za Nidhamu za TFF.

Adhabu zote zinakwenda kwa pamoja, na faini ilipwe ndani ya siku 30.

Bw. Dennis Shemtoi ambaye pia ni Kiongozi wa Arusha FC naye amepewa Onyo na kutozwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) baada ya kutiwa hatiani kwa kutaka kumpiga Mwamuzi katika mechi ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) dhidi ya Arusha United SC iliyofanyika Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha.

Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Ibara za 10(a) na 15(2) za Kanuni za Nidhamu za TFF.

Adhabu zote zinakwenda kwa pamoja, na faini ilipwe ndani ya siku 30 kwa mujibu wa Ibara ya 15(3) ya Kanuni za Nidhamu za TFF.

Kiongozi wa Arusha FC, Bw. Amasha Masenga amepewa Onyo na faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kwa mujibu wa Ibara za 10(a) na 15(2) za Kanuni za Nidhamu za TFF.

Adhabu zote zinakwenda kwa pamoja, faini ilipwe ndani ya siku 30.

Bw. Masenga alilalamikiwa na Bodi ya Ligi kwa kutoa lugha chafu kwenye kikao cha maandalizi ya mechi ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) dhidi ya timu ya Dodoma FC.

Meneja wa Kumuyange FC, Josephat Sinzo amepewa adhabu ya Onyo na faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kwa mujibu wa Ibara za 10(a) na 15(2) za Kanuni za Nidhamu za TFF.

Adhabu zote zinakwenda kwa pamoja, faini ilipwe ndani ya siku 30.

Alilalamikiwa na Bodi ya Ligi kuwa Novemba 11, 2018 katika mehi namba 14 ya Kundi B Ligi Daraja la Pili aliwatolea lugha chafu Msimamizi wa kituo Bw. Mrisho Bukuku pamoja na Mwamuzi.

Mchezaji Dastani D Lipinga wa Mgambo Shooting amefungiwa mechi tatu na faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa mujibu wa Kanuni ya 38(7) ya Ligi Daraja la Kwanza.

Adhabu zote zinakwenda kwa pamoja, faini ilipwe ndani ya siku 30.

Alialamikiwa kuwa Januari 13, 2019 kwenye mechi dhidi ya Geita Gold FC alitaka kumpiga mwamuzi baada ya mchezo huo kumalizika.

Mchezaji Rashid A Shilla wa Mgambo Shooting amefungiwa mechi tatu na faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa mujibu wa Kanuni ya 38(7) ya Ligi Daraja la Kwanza.

Adhabu zote zinakwenda kwa pamoja, faini ilipwe ndani ya siku 30.

Alilalamikiwa kuwa Januari 13, 2019 kwenye mechi dhidi ya Geita Gold FC alimpiga kichwa Meneja wa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi wakati timu zinaingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.

Mtunza Vifaa (Kit Man) Alimu Hadji wa Mashujaa FC amefungiwa kujihusisha na shughuli za mpira wa miguu kwa miezi mitatu (3) na faini ya sh. 200,000 (laki mbili) kwa mujibu wa Kanuni ya 42(2) ya Ligi Daraja la Kwanza.

Adhabu zote zinakwenda kwa pamoja, faini ilipwe ndani ya siku 30.

Alilalamikiwa kuwa 03/11/2018 katika Uwanja wa Mwakangale, Mbeya akishirikiana na Daktari wa timu yake alivamia uwanja kwenye eneo la kuchezea (pitch) kwa lengo la kutaka kuwapiga waamuzi.

Daktari Adamu Maftar wa Mashujaa FC amefungiwa kujihusisha na shughuli za mpira wa miguu kwa miezi mitatu (3) na faini ya sh. 200,000 (laki mbili) kwa mujibu wa Kanuni ya 42(2) ya Ligi Daraja la Kwanza.

Adhabu zote zinakwenda kwa pamoja, na faini ilipwe ndani ya siku 30.

Alilalamikiwa kuwa 03/11/2018 katika Uwanja wa Mwakangale akishirikiana na Mtunza Vifaa alivamia uwanja eneo la kuchezea (pitch) kwa lengo la kutaka kuwapiga waamuzi.

Meneja wa Transit Camp, Bw. Moshi Hamisy amefungiwa kujihusisha na shughuli za mpira wa miguu kwa miezi sita (6) na faini ya sh. 200,000 (laki mbili) kwa mujibu wa Kanuni ya 42(2) ya Ligi Daraja la Kwanza.

Adhabu zote zinakwenda kwa pamoja, na faini ilipwe ndani ya siku 30.

Alilalamikiwa kuwa tarehe 10/11/2018 katika mechi namba 31, kundi B Ligi Daraja la Kwanza dhidi ya Green Warriors iliyofanyika Uwanja wa Azam Complex aliingia uwanjani na kumsukuma mwamuzi.

Kocha Msaidizi wa Transit Camp, Bw. Thomas Gama amefungiwa kujihusisha na shughuli za mpira wa miguu kwa miezi mitatu (3) na faini ya sh. 200,000 laki mbili) kwa mujibu wa Kanuni ya 42(2) ya Ligi Daraja la Kwanza.

Adhabu zote zinakwenda kwa pamoja, na faini ilipwe ndani ya siku 30.

Alilalamikiwa kuwa tarehe 10/11/2018 katika mechi namba 31, kundi B Ligi Daraja la Kwanza dhidi ya Green Warriors iliyofanyika Azam Complex alifanya vurugu kwa kutokubaliana na maamuzi aliyoyatoa mwamuzi wa mchezo.

Kiongozi wa Transit Camp, Bw. Santos Kato amefungiwa kujihusisha na shughuli za mpira wa miguu kwa miezi mitatu (3) na faini ya sh. 200,000 (laki mbili) kwa mujibu wa Kanuni ya 42(2)ya Ligi Daraja la Kwanza.

Adhabu zote zinakwenda kwa pamoja, faini ilipwe ndani ya siku 30.

Alilalamikiwa kuwa tarehe 10/11/2018 katika mechi namba 31, kundi B Ligi Daraja la Kwanza dhidi ya Green Warriors iliyofanyika Azam Complex alianzisha vurugu na kusababisha mchezo kusimamishwa.

Baadae alipelekwa jukwaa kuu lakini aliendelea na vurugu hizo.