Mabingwa wa Cosafa,Timu ya Taifa ya Wanawake U20 “Tanzanite” imewasili ikitokea Port Elizabeth,Afrika Kusini ilipokua ikishiriki mashindano ya Cosafa.

Tanzanite imetua saa 1 na nusu usiku ikiwa na Kombe la Ubingwa wa mashindano hayo pamoja na medali za dhahabu.

Mapokezi yaliongozwa na Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Juliana Shonza ambaye amewapongeza Wachezaji kwa kufanikiwa kunyakua ubingwa ambao unaipa heshima nchi.

Viongozi wengine waliokuwepo ni Rais wa TFF Wallace Karia aliyeongozana na Makamu wake Athuman Nyamlani,Katibu Mkuu Kidao Wilfred,na viongozi wengine wa Serikali,BMT na TFF.

Baada ya mapokezi hayo Rais wa TFF Wallace Karia na Makamu wake Athuman Nyamlani waliongozana na Kikosi hicho mpaka Hotelini ambako walikula pamoja chakula cha usiku ambapo Rais Karia amewataka Wachezaji wa Kikosi hicho kuendeleza juhudi na kujitunza hata watakaporudi majumbani kwao na kwenye klabu zao.

Amesema TFF itahakikisha inaendelea kuwatengenezea mazingira bora na kuendeleza vipaji vyao.

Naye Nahodha Msaidizi Opa Clement ameishukuru TFF na kumuhakikishia Rais wa TFF kuwa wataendelea kujitunza na kupigania Taifa wakati wowote wakipata nafasi.

Katika mashindano ya Cosafa yaliyoanza Agosti 1-11,2019 Tanzanite ilikua katika Kundi B ambapo ilipata ushindi mechi mbili 2-0 dhidi ya Botswana,8-0 dhidi ya Eswatini na kupoteza mchezo mmoja na Zambia kwa mabao 2-1.

Ilipata ushindi nusu fainali dhidi ya Afrika Kusini wa mabao 2-0 kabla ya kuifunga Zambia 2-1 katika mchezo wa fainali iliyochezwa jana Uwanja wa Wolfson.

Mbali na Kombe Tanzanite wamepata medali za dhahabu huku Nahodha Enekia Kasonga akiibuka kuwa mchezaji Bora wa Mashindano.

Katika hatua ya makundi Diana Msemwa alifanikiwa kuibuka na tuzo mbili za mchezaji bora wa mchezo katika mchezo dhidi ya Botswana na mchezo dhidi ya Eswatini huku Aisha Masaka akifanikiwa kuondoka na mpira baada ya kufunga mabao 3 kwenye mchezo dhidi ya Eswatini.