Mafunzo ya Uongozi na Usimamizi Katika Soka la Wanawake Yahitimishwa Rasmi Mkoani Tanga na Kuelekea Arusha

Kozi ya Uongozi na Usimamizi katika masuala ya mpira wa miguu kwa upande wa wanawake iliyofanyika Jijini Dar es Salaam imeendelea kutolewa Jijini Tanga ambapo washiriki 25 walipata nafasi ya kuhudhuria na kupatiwa mafunzo hayo yanayoratibiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) chini ya mwamvuli wa FIFA.

Akifunga mafunzo hayo yaliyochukuwa muda wa takribani siku tano, Ofisa Michezo wa Mkoa wa Tanga Ndugu, Digna Tesha aliushukuru uongozi wa TFF ulio chini ya Rais Karia kwa kuwapa nafasi ya upendeleo wakazi wa Jiji la Tanga na kuwafanya kuwa wanufaika wa pili wa mradi huo baada ya kuanzia Dar es Salaam.

Ofisa huyo aliongeza kuwa wao kama wakazi wa Tanga wana kila sababu ya kujivunia uwepo wa TFF, kwa kuwa imekuwa ni kati ya wadau wa maendeleo ya soka Jijini hapo na kwamba mafunzo hayo pia yatakwenda kuamsha hamasa na kutia chachu zaidi ya maendeleo ya mpira wa miguu wa wanawake mkoani humo ; kwani wahitimu wa kozi hiyo muhimu ya uongozi na usimamizi katika masuala ya soka la wanawake watakwenda kuchangia kueneza elimu hiyo kwa wadau wengine.

Katibu Mkuu wa TFF Kidao Wilfred alisema kuwa lengo kuu la mafunzo hayo ni kueneza na kuendeleza elimu ya uongozi na usimamizi wa soka katika mikoa mbalimbali ili kuzidi kuwajengea uwezo zaidi na kuhakikisha kuwa soka la wanawake nalo linakuwa na wasimamizi, madaktari, waamuzi na makocha wanawake pia.

Kidao aliongeza kuwa mpango wa kuwajengea uwezo wanawake katika Nyanja mbalimbali ni mpango maalum unaotambuliwa na FIFA na kwamba kwa sasa FIFA imeweka kipaumbele kikubwa zaidi katika soka la wanawake hivyo TFF ili kuendana na kasi hiyo nayo imeamua kuanza kuweka mikakati tofauti tofauti ya kuendeleza mafunzo ya kada nyingi kuliko ilivyowahi kutokea.

Kuhusu kuchagua ama kupeleka mafunzo hayo pembezoni mwa mikoa na majiji; Kidao alieleza kuwa hiyo ilikuwa ni hatua ya awali tu ambayo imeanzia katika makao makuu ya mikoa husika na kadri siku zinavyokwenda wanaweza kupanua wigo hadi vijijini na kwamba ni suala la kimkakati tu.

Hata hivyo Katibu Kidao alibainisha kuwa kupeleka mafunzo hayo katika majiji mbalimbali na katika makao makuu ya mikoa inatagemeana na uamuzi wa wenyeji wa eneo husika kwani hakuna kigezo kinacholazimisha mafunzo hayo kufanyikia mikoani ama sehemu nyinginezo.

Tukio la kufungwa kwa kozi hiyo lilihudhuriwa na Bi Digna Tesha (Mgeni Rasmi) Katibu Mkuu wa TFF Kidao Wilfred, Mjumbe wa Kamati Tendaji ya TFF (EXCOM) Khalid Mohammed, Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tanga Said Soud, Ofisa Michezo Jiji la Tanga Michael Monica Njaule, Katibu wa chama cha soka Tanga Betris Mgaya na Mkufunzi wa mafunzo hayo Daktari Henry Tandau.

Mafunzo hayo yaliyozinduliwa rasmi Dar es Salaam 15-19 Septemba, tarehe 21-25 Septemba, 2020 yakaenda Tanga na kuanzia Septemba 28 hadi Oktoba 02 2020 yamekuwa yakiendelea mkoani Arusha kisha baada ya Arusha Dodoma, Unguja, Mwanza, Geita, Kigoma, Mbeya, Songea huku hapo baadaye yakitarajiwa kufika mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani.