Makocha 29 wawania Diploma C ya CAF

Makocha 29 kutoka sehemu mbalimbali nchini wanashiriki katika kozi ya diploma C ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) iliyoanza Machi 29 mwaka huu mkoani Morogoro.

Akifungua kozi hiyo ya nadharia na vitendo itakayofanyika kwa miezi mitatu, Makamu wa Pili wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Steven Mnguto aliwataka washiriki kuzingatia mafunzo ili kutimiza lengo ambalo ni kukuza mpira wa miguu wa Tanzania.

Mnguto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), pia aliwataka makocha hao wanapopata kazi katika klabu mbalimbali kuwa na misimamo katika kazi yao, kwani ukocha ni taaluma kama zilivyo nyingine.

Alisema iwapo wote watafanya vizuri katika kozi hiyo na kufanya kazi yao ya ufundishaji mpira wa miguu kwa weledi itasaidia kuondoa wimbi la makocha wa kigeni nchini.

Aliongeza kuwa TFF iko tayari kutoa mchango wake kwa makocha utakapohitaji ili kusogeza mbele taaluma hiyo, kwani ina nafasi kubwa katika maendeleo ya mpira wa miguu nchini.

Mafunzo hayo yanayofanyika katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) chini ya Wakufunzi Sunday Kayuni na Oscar Mirambo yamegawanyika katika awamu sita za nadharia na vitendo.