Mashindano ya CECAFA U-18 kuanza kesho Julai 25, 2023

Mashindano ya CECAFA kwa wanawake wenye umri chini ya miaka 18 yataanza rasmi kesho Julai 25, 2023 katika uwanja wa Azam Complex, Chamazi ambapo Tanzania itatupa karata yake ya kwanza dhidi ya timu ya Burundi majira ya sa 9 kamili Alasiri.

Mashindano hayo yanajumuisha nchi tano kutoka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ambazo ni Uganda, Ethiopia, Burundi, Zanzibar na Tanzania ambaye ni mwenyeji wa mashindano hayo kwa mwaka huu.

Akizungumza kuelekea katika mashindano hayo kocha mkuu wa timu ya Tanzania U-18 Bakari Shime alisema, maandalizi yote yamekwenda vizuri na wachezaji wote wako tayari kwa mashindano.

“Timu imepata muda mrefu wa kujiandaa na mashindano ya CECAFA kutokana na kuahirishwa kwa zaidi ya mara mbili kwa mashindano hayo ambapo hapo awali yalipangwa kufanyika Kenya, hivyo nina imani wachezaji watakwenda kuonyesha viwango bora na ushindani wa hali ya juu” alisema Kocha Shime.

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake Hasnat Ubamba alisema wao kama wachezaji wamejiandaa kufanya vizuri katika mashindano ya CECAFA huku akiwaomba watanzania kuendelea kuwaunga mkono na kujitokeza kwa wingi katika uwanja wa Azam Complex kuishangilia timu yao.