TFF ya Farijika na Hamasa  Kutoka kwa Mashabiki na Wanahabari wa Soka Nchi

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania ndugu, Kidao Wilfred amesema amefarijika na umati mkubwa uliojitokeza katika kushuhudia mchezo wa kirafiki  kati ya wandishi wa habari waliooa na wale wasiooa uliofanyika  leo 31 Mei, 2020 kwenye viwanja vya Shule Kuu ya Sheria Mawasiliano, Ubungo- Dar es Salaam; ambapo timu ya wasiooa wameibuka washindi kwa mikwaju ya penati 4-1 baada ya muda wa kawaida kumalizika pasipo mbabe.

Katibu Kidao amesema amepata faraja pia kwa wanahabari hao kuandaa mashindano hayo na kumualika kuwa mgeni rasmi akiiwakilisha TFF inayoongozwa na Rais Wallace Karia.

Kidao ameongeza kuwa mashindano hayo si Burudani tu, bali ni sehemu ya uzinduzi wa kurejea kwa ligi Tanzania Bara ambazo zilikuwa zimesimama tangu kuingia kwa virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa wa hatari wa Covid -19 uliogundulika kwa mara ya kwanza China Mnamo Novemba 2019 na kuingia Tanzania katikati ya mwezi Machi, 2020.

Akikabidhi kombe kwa washindi wa mashindano hayo, Kidao amewapongeza wachezaji wa pande zote mbili na kusema kuwa mashindano kama hayo yanaimarisha umoja na afya za watanzania, kwani ni sehemu ya mazoezi kwa waandishi ambao kwa msingi wao shughuli yao kuu ni kupasha habari, kuburudisha na kuelimisha jamii kupitia kalamu, TV na redio.

Pamoja na Burudani hiyo ya mpira kuruhusiwa na Mh. Daktari, John. P. Magufuli na kurejea, Kidao amewataka wanahabari wawe mabalozi wazuri kuielimisha jamii na mashabiki wa soka kuzingatia miongozo yote inayotolewa na wataalam wa afya na serikali pia ili kujilinda na kuwalinda wengine dhidi ya kusambaza na kueneza Virusi vya Corona.

Kocha wa kikosi cha mabachela, Haji Sunday Manara ambaye pia ni msemaji wa klabu ya Simba, amedai kuwa alijua kuwa kikosi chake kingeibuka na ushindi hata kabla ya kuianza mechi; licha ya wapinzani wake kutangulia kupata mabao mawili bado Manara aliamini kuwa ushindi u mikononi mwa masela hao.

Naye kocha msaidizi wa kikosi cha waliooa Omari Katanga amezisifia mbinu walioitumia wapinzani wake mpaka kufanikiwa kurejesha magoli hayo na hatimaye kuibuka na ushindi huku akisema  kuwa mashindano hayo yalikuwa mazuri licha ya kikosi chake kukubali kupata kichapo. Pamoja na kuwa kikosi hicho kilitangulia kupata magoli 2 katika kipindi cha kwanza   baadaye magoli hayo yalirudishwa na hivyo kupelekea mchezo huo kuamliwa kwa penati.

Katika hatua hiyo ya matuta, masela waliweza kupachika mikwaju 4 huku wale wanaopikiwa na kuchemshiwa maji na wenziwao wakiambulia penati moja iliyopigwa na mchezaji mkongwe wa klabu ya Yanga Ali Mayai (Tembele) aliyetamba miaka hiyo; je wajua chanzo cha waliooa kupatiwa kichapo hicho?   Fuatilia habari zetu laini.