Michuano ya COSAFA Yaanza Kurindima Durban, Afrika Kusini.

Michano ya COSAFA kwa upande wa Soka la Ufukweni (Beach Soccer) imeanza kutimua vumbi rasmi Novemba 17, 2021 katika fukwe za jiji la Durban zilizopo Afrika ya Kusini ndani ya viwanja vya ‘South Beach’ (Fukwe za Kusini).

Michuano hiyo imejumuisha timu mbalimbali kutoka ukanda wa COSAFA Kusini mwa Afrika, kama vile; Angola, Comoros, Mozambique, Seychelles, Afrika ya Kusini na Tanzania licha ya Madagascar kutokuweza kushiriki kutokana na changamoto mvalimbali, bado ratiba ya michuano imeendelea kama kawaida.

Katika michuano hiyo, Beach Stars ya Tanzania ameshiriki kama timu alikwa ikitokea Ukanda wa Afrika Mashariki.

Mchezo wa kwanza na wa ufunguzi wa mashindano hayo uliwakutanisha wenyeji Afrika ya Kusini dhidi ya Seychelles, mchezo uliowatoa kifua mbele wenyeji Afrika ya Kusini kwa ushindi wa 4-2, huku Seychelles ikiyaanza mashindano hayo vibaya kwa kupoteza mchezo huo.

Katika mchezo wa pili uliowakutanisha Mozambique dhidi ya Comoros ambao ulimalizika kwa Mozambique kupata matokeo mazuri baada ya kuwadhibu vikali wapinzani wao kwa goli 8-3 na hivyo kufanya ratiba ya siku ya kwanza kumalizika kwa michezo hiyo miwili ya kukata utepe.

Novemba 18, 2021 timu ya Soka la Ufukweni ya Tanzania ‘Beach Stars’ itashuka dimbani kutupa karata yake ya kwanza kwa michezo miwili ambapo mchezo wa kwanza utakuwa dhidi ya Mozambique (Msumbiji) huku mchezo wake wa pili ukiwakutanisha na timu ya Comoros.

Kuelekea michezo ya hiyo, kocha wa timu ya Taifa ya Tanzania ya soka la ufukweni (Beach Stars), Boniface Pawasa alisema: “Awali ya yote tunamshukuru Mungu kwa kufika siku ya leo pamoja na maandalizi mazuri kutoka katika uongozi wa TFF. Kiufundi kikosi kipo katika hali nzuri mawazo na akili zetu zote tumeelekeza kupambana katika siku ya kesho kulinda heshima ya nchi yetu na tuna amini kuwa kupitia kutazama michezo ya wapinzani wetu hii leo imetupa picha kwamba ni watu wa namna gani tunaenda kukutana nao; na tunaamini tunafanya vizuri. “ Alisema Pawasa.

Sambamba na hayo siku hiyo ya Novemba 18, 2021 kutakuwa na mchezo utakao wakutanisha Angola dhidi ya Seychelles; na badaye wenyeji Afrika ya Kusini itakutana na Angola.