MSHAMBULIAJI wa timu ya Simba ya Dar es Salaam, Miraji Athumani amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Septemba wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu wa 2019/20, huku Patrick Aussems pia wa Simba akichaguliwa Kocha Bora wa mwezi huo.
Miraji na Aussems walitwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzao walioingia nao fainali katika uchambuzi uliofanywa Dar es Salaam wiki hii na Kamati ya Tuzo ya VPL inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutokana na mapendekezo kutoka kwa makocha waliopo viwanja mbalimbali, ambavyo ligi hiyo inachezwa msimu huu.
Kwa mwezi huo wa Septemba, Simba ilicheza michezo mitatu na kushinda yote ikiifunga Mtibwa Sugar mabao 2-1, Kagera Sugar mabao 3-0 na Biashara United mabao 2-0, ambapo Miraji alikuwa na kiwango kizuri uwanjani kwa mwezi huo akichangia kwa asilimia kubwa mafanikio hayo ya Simba ikiwa ni pamoja na kufunga mabao mawili na kutoa pasi za mabao mawili.
Miraji aliwashinda Meddie Kagere wa Simba aliyetoa mchango mkubwa pia katika mafanikio ya Simba ikiwa ni pamoja na kufunga mabao manne. Mchezaji mwingine aliyeingia fainali alikuwa Ismail Kada wa Prisons aliyeonesha kiwango kizuri na kutoa mchango katika michezo ambayo Prisons ilicheza ikishinda miwili, sare mmoja, ambapo iliifunga Ruvu Shooting mabao 2-1, Mtibwa Sugar mabao 3-1 na kutoka sare na Lipuli mabao 2-2.
Kwa kutwaa tuzo hiyo, Miraji atazawadiwa kikombe na Tsh. 1,000,000 (milioni moja) kutoka Vodacom. Vilevile atapata Kisimbusi kutoka Azam TV.
Kwa upande wa Aussems aliwashinda Mohammed Rishard wa Prisons na Abdallah Mohammed Baresi wa JKT Tanzania, ambapo Aussems aliongoza timu yake kupata ushindi katika michezo mitatu, kati ya hiyo mmoja nyumbani dhidi ya Mtibwa Sugar na miwili ugenini mabao 3-0 dhidi ya Kagera Sugar na mabao 2-0 dhidi ya Biashara United. Simba imemaliza mwezi ikiwa nafasi ya kwanza.
Rishard aliingia hatua ya fainali baada ya kuiongoza Prisons kushinda michezo miwili na kutoa sare mmoja, ambapo ilishinda nyumbani mabao 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting, kisha ikashinda ugenini mabao 3-1 dhidi ya Mtibwa na ikatoka sare ugenini na Lipuli ya mabao 2-2, wakati Baresi aliingoza JKT Tanzania kushinda michezo miwili, sare moja na kupoteza mmoja.
JKT Tanzania ilifungwa ugenini bao 1-0 na Lipuli, ikatoka 0-0 nyumbani na Mtibwa Sugar, ikashinda bao 1-0 ugenini dhidi ya Biashara United na pia ikapata ushindi ugenini kama huo dhidi ya Kagera Sugar