Mkurugenzi wa mashindano Salum Madadi atoa muongozo kwa viongozi ligi daraja la kwanza ya wanawake

Mkurugenzi wa mashindano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Mwalimu Salum Madadi atoa maelekezo kwa viongozi na makocha wa ligi ya wanawake ya daraja la kwanza kuelekea hatua ya mtoano (robo fainali).

Mkurugenzi Madadi alitoa maelekezo hayo katika kikao cha maandalizi ya kwenda katika hatua ya robo fainali kilichofanyika (03 Septemba, 2020) alipokuwa akizungumza na baadhi ya viongozi na makocha wa timu zilizobahatika kufuzu kuingia katika hatua hiyo ambayo ilikuwa ikigombaniwa na takribani timu 16 za daraja la kwanza.

Akitoa muongozo huo kwa makocha na baadhi ya viongozi wa timu waliohudhuria kikao hicho, Mwalimu Madadi alisema kuwa anaimani kubwa na mashindano yaliyofanyika mpaka kufikia hatua ya robo fainali na kwamba hana shaka na timu zilifuzu kwenda hatua ya mtoano.

Aidha, Mwalimu Madadi aliweka bayana baadhi ya mambo muhimu kwa kusema kuwa mashindano hayo ya ligi daraja la kwanza ya wanawake yanamalengo ya kupata pia wachezaji watakao weza kuunda timu ya Taifa ya wanawake huku akitaja kuwa mpaka sasa kuna wachezaji watatu ambao wamekwisha pendekezwa na makocha wa timu za Taifa za wanawake kutoka timu ambazo hazikufuzu kuendelea katika hatua ya mtoano. Hivyo, wachezaji hao watapaswa kubaki hapo hapo Fountain Gate Academy kwa ajili ya kusubiria usahili utakao endelea baada ya kukamilika kwa michuano hiyo tarehe 06 Septemba, 2020.

Mwalimu Madadi pia aliwataka viongozi wa timu za wanawake pamoja na wachezaji wote kujipa moyo kuwa wao wanaweza na hivyo wasiwe wenye kukata tamaa, kwani ligi ya wanawake ndio kipaumbele mama hata kwa FIFA; hivyo, hawana budi kutembea kifua mbele wakifahamu ya kuwa mpira wa wanawake ni sawa tu na mpira wa wanaume na kwamba tofauti iliyopo ni njinsia pekee.

Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa ligi ya wanawake sio bonanza isipokuwa ni mashindano kamili kama yalivyo mashindano mengine ya mpira wa wanaume; na katika msimu ujao TFF inataraji kuyaboresha zaidi ili kuongeza mvuto kwa wadau wa soka kwa ujumla.

Zaidi ya hapo, mwalimu Madadi alieleza kuwa katika timu zitakazo ipeleka nchi hii katika mafanikio ya soka ya haraka ni ya wanawake; kwa kuwa tayari Tanzania imekwisha kutambulika kupitia soka la wanawake na sasa ikiwezekana Tanzania inaweza kushiriki michuano hata ya kombe la dunia kwa wanawake kabla ya ile timu ya wanaume.

 

 

 

 

//////////////////////////////////The End///////////////////////////////////////////////

Meneja wa mashindano wa TFF Baraka Kizuguto aanika ratiba ya hatua ya mtoano ligi daraja la kwanza

Uongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania umetoa ratiba ya hatua ya mtoano (robo fainali) ligi daraja la kwanza ya wanawake uliyozihusisha timu nane pekee ambazo zilizofuzu kuingia katika hatua hiyo kati ya timu 16 za awali.

Akizungumza na baadhi ya viongozi wa timu na makocha waliohudhuria mkutano huo, meneja wa mashindano wa TFF Baraka Kizuguto alifafanua ratiba ya hatua ya mtoano ambayo itaanza tarehe 04 Septemba, 2020 ambapo mechi nne zote zitachezwa katika uwanja mmoja wa Fountain Gate Arena kuanzia saa 02:00 asubuhi mpaka saa 10:00 jioni.

Baraka Kizuguto ametoa maelekezo kuhusu suala la nidhamu na namna ambavyo viongozi wa timu wanavyopaswa kuzingatia kanuni na taratibu zote zinazoongoza mpira wa miguu nchini na duniani kote kwa kusema kuwa sheria zinazotumika katika ligi daraja la kwanza kwa wanawake ni zile zile zitumikazo katika ligi zote. Kwa hiyo kama mchezaji anakadi za onyo 3, hataruhusiwa kucheza mchezo unaofuata kwa namna yeyote ile.

Kizuguto alieweka bayana kuwa suala la nidhamu kwa timu na viongozi na makocha si la hiari bali ni faradhi kwao kuhakikisha nidhamu inazingatiwa ndani na nje ya uwanja na kwamba utovu wa nidhamu unaweza kupelekea timu kunyang’anywa alama na kupewa adhabu kwa mujibu wa kanuni na taratibu za TFF. Hivyo ni lazima timu na viongozi wote kuzingatia suala la nidhamu kama ndio msingi wa mafanikio yao.

Kizuguto alikemea vikali tabia ya baadhi ya timu kuingiza wachezaji wengine wasio kuwa na sifa za kucheza ligi daraja la kwanza kificho; na kueleza kuwa suala hilo si la kiungwana na hivyo kwa yeyote atakayeshiriki kufanya hivyo atua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake.

Mwisho meneja Kizuguto  aliweka wazi kuwa mchezo wa kwanza utakuwa kati ya Mpinduzi Queens ya Njombe na Amani Queens ya Lindi saa 2:00 asubuhi; mechi ya pili itawakutanisha ES Unyanyembe ya Tabora na Moskisa Queens  ya Kilimanjaro saa 04:00 asubuhi; mchezo wa tatu utakuwa ni kati ya Mkwawa Queens ya Iringa dhidi ya  Evergreeen ya Dar es Salaam huku Ilala Queens na Shinyanga Super Queens wakikamilisha  ratiba.

Baada ya michezo hiyo, mechi za nusu fainali zitachezwa siku ya Juma pili michezo hiyo ambayo ndiyo inatrajiwa kuwapata washindi wawili watakaopanda kwenda ligi kuu ya wanawake ijulikanayo kama Ligi ya Wanawake ya Serengeti Lite ya Tanzania Bara.( Serengeti Lite Women Premier League)