Mtibwa Sugar Bingwa Tena Ligi kuu U-20

Mtibwa sugar imefanikiwa kutetea ubingwa wake wa ligi kuu ya vijana chini ya umri wa miaka 20 kwa msimu huu wa 2021/2022 baada ya kuifunga timu ya Mbeya Kwanza kwa magoli goli 4-1 kwenye mchezo wa fainali uliopigwa Julai 17, 2022 majira ya 11:00 jioni Katika dimba la Azam Complex Chamazi.

Hii ni mara ya nne mfululizo kwa timu hiyo kubeba Kombe hilo la ligi kuu ya vijana (U-20) katika mashindano yanayo andaliwa na kusimamiwa na TFF.

Kocha wa Mtibwa Sugar Awadh Juma alisema “tunamshukuru Mungu kwa kutwaa ubingwa kwa mara nyingine tena, niipongeze timu yangu kwa kufanya vizuri na niipongeze TFF kwa maandalizi mazuri na kuratibu vizuri ligi hii kwani imekuwa na ushindani wa aina yake ukilinganisha na mwaka uliopita. Tumeona vipaji vingi na vichanga ambavyo vikiendelezwa vitakuwa na mchango mkubwa kwa vilabu vyetu.”

Mabao ya Mtibwa Sugar yalifungwa na Ezekiel Eusebio dk 20, Ladack Chasambi dk 45, Said Mkopi dk 84 na Omary Suleiman dk 90 wakati goli pekee la Mbeya Kwanza likifungwa na Willie Thobias dk ya 68.

Timu ya Mtibwa sugar imefanikiwa kutoa golikipa bora ambaye ni Razack Shekimweli, Mchezaji bora Ladack Chadambi na kocha Bora wa ligi akiwa ni Awadh juma. Tuzo zingine zilizotolewa ni mwamuzi bora iliyochukuliwa na Kelvin Martin, mwamuzi msaidizi ikibebwa na Tumaini Kimaro.

Mchezo mwingine uliopigwa kwenye fainali hizo ni mchezo wa kusaka mshindi wa tatu ambao ulimalizika kwa Azam FC kuifunga Coastal Union kwa penati 4-3 baada ya dk 90 kutamatika kwa sare ya 1-1.