Mtibwa Sugar Bingwa TFF U20 Ligi

Ligi Kuu ya Vijana wa U-20 imefikia tamati Julai 2, 2023 kwa timu ya Vijana ya Mtibwa Sugar kutwaa ubingwa huo kwa mara ya tano mfululizo.

Mtibwa Sugar ilifanikiwa kupata ubingwa huo baada ya kuifunga timu ya Geita Gold bao 1-0 kwenye mchezo wa fainali uliopigwa katika uwanja wa Azam Complex Chamazi majira ya saa 12:00 ambapo licha ya kutwaa ubingwa bado ilikutana na upinzani mkubwa kutoka kwa vijana wa Geita.

Dakika 90 pekee hazikutosha kumaliza mchezo huo wa fainali ambapo ndani ya dakika 90 za kawaida hakuna timu iliyofanikiwa kuandika bao lolote, jambo lililopekea mchezo huo kwenda hadi dakika 120 baada ya kuongeza dakika 30.

Aidha, katika dakika ya 7 za kwanza kwenye dakika 30 za muda wa ziada mshambuliaji kinara wa mabao wa Mtibwa Sugar, Athumani Makambo alifanikiwa kuwapatia bao la kuongoza (dkk 97) ya mchezo, bao hilo likidumu mpaka fainali inamalizika.

Athumani Makambo (Mtibwa), alifanikiwa kuibuka kinara wa upachikaji mambao akitupia jumla ya mabao (7), akifuatiwa na Cyprian Kachwele wa Azam FC, huku Razaq Chasambi (Mtibwa) akinyakua tuzo ya mchezaji bora wakati Topa Ushindi naye akiibuka goli kipa bora wa U-20.

Makambo anaendelea kuweka rekodi yake katika michuano ya vijana kwani hata wakati anashiriki michuano ya U17 alikuwa Miongoni mwa vinara wa upachikaji mabao.

Baada ya mchezo huo Awadh Juma, kocha wa Mtibwa Sugar aliwapongeza wachezaji wake kwa kupambana hadi kutwaa ubingwa huo tena. Alisema haikuwa kazi ndogo kufikia hapo kutokana na ubora uliooneshwa na Geita Gold katika fainali hiyo huku pia akitoa sifa kwa timu zote zilizoshiriki kwa kuonesha viwango bora kwenye Michuano hiyo.

Naye Choke Abeid, kocha wa kikosi cha Geita Gold alisema kuwa mchezo huo wa fainali ya U20 ulikuwa mgumu kwa pande zote na kwamba wachezaji wake walifanya makosa machache yakawaadhibu lakini bado walikuwa katika ubora wa hali ya juu. Hata hivyo, Kocha huyo alitoa pongezi kwa Mtibwa Sugar kwa mchezo waliouonesha lakini pia kwa kutwaa ubingwa huo kwa mara ya tano mtawalia.

Mtibwa Sugar iliingia kwenye hatua hiyo ya Fainali baada ya kuwatoa Azam FC huku Geita Gold wao wakitinga hatua hiyo kwa kuwatoa Kagera Sugar katika hatua ya nusu fainali; timu zote 4 zikicheza michezo yao ya nusu fainali Juni 30, 2023 hapo hapo Chamazi. Azam wao waliambulia nafasi ya tatu huku vijana wa Kagera Sugar wao wakishika nafasi ya nne.