MTIBWA WATINGA FAINALI YA 3 MFULULIZO:

Mabingwa watetezi wa U20 Premier League Mtibwa Sugar ya Turiani mkoani Morogoro imeingia fainali ya michuano ya vijana kwa vilabu vya ligi kuu wenye umri chini ya miaka 20 baada ya kuwafunga Simba Sc ya jijini Dar es salaam kwa magoli 3-1 katika mchezo wa nusu fainali ya pili uliochezwa kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar.
Mtibwa Sugar ambao wanawania kulibeba kombe hilo kwa mara ya tatu mfululizo walianza kwa kuwa mabingwa mwaka 2018 jijini Dodoma na kufanya hivyo tena mwaka 2019 jijini Dar, michuano hiyo haikufanyika mwaka jana (2020) kutokana na changamoto ya ugonjwa wa COVID-19.
Iwapo itafanikiwa kulibeba kombe hilo itakuwa ni timu ya kwanza kufanya hivyo (kuchukua mara tatu mfululizo).
Katika fainali itakayochezwa siku ya Jumamosi saa moja usiku mabingwa hao watetezi watacheza na timu ya Yanga Sc ambao wameingia fainali kwa kuiondosha timu ya Azam Fc kwa mikwaju ya penati. Timu hiyo ya Yanga ilicheza mchezo wa fainali kwa mara ya mwisho mwaka 2013 (Uhai Cup) na kupoteza kwa Coastal Union, bila shaka na wao watataka kuonyesha kwamba msimu huu wamedhamiria kubeba kombe tofauti na Msimu uliopita (2019) ambao walishika nafasi tatu kwa kumfunga mtani wake Simba Sc.
Katika hatua nyingine mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu utachezwa siku hiyohiyo ya Jumamosi na utaanza majira ya saa kumi kamili alasiri (1600hrs) kati ya Azam Fc dhidi ya Simba Sc.
Baada ya mchezo wa fainali kutakuwa na matukio mbalimbali ya ugawaji wa zawadi kwa wachezaji na timu ambazo zitakuwa zimefanya vizuri katika maeneo tofauti tofauti.