Namungo Yaivuta Shati Young Africans Ilulu Lindi

Mchezo kati ya Namungo FC na Young Africans umemalizika kwa timu hizo kutoka sare ya kufungana bao moja kwa moja huku Namungo wakimaliza dakika tisini (90) wakiwa pungufu baada ya mchezaji wao Alpha Nyenye kuoneshwa kadi ya njano mbili zilizopelekea kupatiwa kadi nyekundu katika kipindi cha lala salama.

Mchezo huo uliopigwa Novemba 20, 2021 kwenye uwanja wa Ilulu uliopo Lindi Mijini ulikuwa mkali na wenye ushindani mkubwa ambapo timu hizo zikishindwa kufungana katika kipindi cha kwanza cha mtanange huo licha ya Namungo kutengeneza nafasi kadhaa ambazo endapo Chiza Kichuya angetulizana huenda Namungo wangeweza kuandika bao la mapema zaidi lakini hali haikuwa hivyo hadi kipindi cha awali kinamalizika.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kufanya mashabulizi makali, na kunako dakika ya 53 Namungo wakafanikiwa kupata bao la kuongoza kupitia kwa Obrey Chirwa nyota wa zamani wa Young Africans na Azam FC kabla ya Young Africans nao kusawazisha bao hilo kupitia mkwaju wa penati; iliyopigwa na Saido Ntibazonkiza na kuufanya mchezo huo kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Kocha Msaidizi wa Namungo FC Godfrey Onkonko alisema kuwa kikosi chake kimepambana na kwamba kilijiandaa vyema kuhakikisha kinaondoka na alama tatu kwenye mchezo huo, lakini haikuwa bahati kwao kwani walifanikiwa kutengeneza nafasi nyingi za magoli na kushindwa kuzitumia ipasavyo; endapo zingetumika vizuri basi wangeweza kuibuka na ushindi katika mchezo huo uliokuwa na upinzani mkubwa kwa pande zote.

Kocha huyo wa Namungo aliongeza na kusema kuwa mchezo huo umekwisha na kwamba wanakwenda kujipanga kwa ajili ya michezo mingine ya Ligi kwani anafahamu kwamba ligi ya mwaka huu inaupinzani mkubwa; hivyo timu itakayojipanga vyema ndiyo itakayopata matokeo huku akikubali matokeo hayo na kusema huo ndio mpira.

Kwa upande wake kocha Msaidizi wa Young Africans Cedric Kaze yeye alisema kuwa kikosi chake kimecheza vyema licha ya kushindwa kuonesha kiwango bora kama ilivyozoeleka hivi karibuni akidai kuwa hali ya uwanja nayo ilichangia wachezaji wake kushindwa kucheza vyema ili kuweza kuondoka na alama zote tatu huku akiongeza kuwa mchezo ulikuwa mgumu na wa kiufundi zaidi.

Aidha,kocha huyo alifafanua kuwa timu yake haikuwa katika kiwango bora wakati wapinzani wao Namungo walionekana kuwa bora zaidi kwani walionesha kuhitaji matokeo kwa nguvu zaidi; suala lililopelekea kuongezeka kwa ushindani kwenye mchezo huo ambao ulikuwa na umuhimu kwa kila timu.

Katika michezo mingine iliyopigwa Novemba 20 kwenye viwanja tofauti tofauti; huko Mbeya Mtibwa Sugar alishindwa kutamba mbele ya Mbeya City baada ya kukubali kipigo cha bao 3-1 huku Geita Gold nao wakifanikiwa kupata ushindi wa kwanza dhidi ya Kagera Sugar mchezo huo ukipigwa kwenye uwanja wa Kaitaba Kagera. Ushindi huo iliyoupata Geita Gold ni wa kwanza tangu timu hiyo ianze kushiriki Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.

Kufuatia matokeo hayo Young Africans inaendelea kuongoza kwa kuwa na jumla ya alama 16 ikiiacha Simba kwa alama mbili pekee, Simba wakiwa katika nafasi ya pili na alama 14, nafasi ya tatu ikienda kwa Mbeya City aliye na alama kumi (10) sawa na Polisi Tanzania na Dodoma Jiji huku Mbeya City akiwa na faida ya mabao ya kufunga na kufungwa.