NBC Yategua Kitendawili cha Udhamini Ligi Kuu Bara
Kitendawili kilichokuwa miongoni mwa wadau wengi wa mpira wa miguu Tanzania kuhusu nani atakuwa mdhamini wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara (TPL) kimeteguliwa Octoba 6, 2021 ambapo Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imetia saini Mkataba wa kudhamini ligi hiyo baada ya kufikia makubaliano na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa udhamini wa kiasi cha Shillingi za Kitanzania bilioni 2.5.
Hafla hiyo fupi ya utiaji saini mkataba huo imefanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency iliyopo Jijini Dar es Salaam ambapo viongozi wa pande zote mbili walikuwepo huku NBC ikiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Theobald Sabi aliyefuatana na wakurugenzi wengine wakati kwa upande wa TFF wao waliongozwa na Rais Wallace Karia.
Mkurugenzi wa NBC alisema, benki hiyo imefikia maamuzi ya kufanya uwekezaji kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuridhishwa na mwenendo bora wa ligi pamoja na thamani ya ligi hiyo kwa sasa. Aliongeza kuwa weledi na umahiri ulioneshwa na uongozi wa TFF katika usimamizi na uangalizi wa sera za soka ndiyo sababu mojawapo iliyoivutia benki hiyo kufanya uwekezaji huo.
Mbali na hayo, Mkurungezi Sabi alitanabaisha ya kwamba utawala unaozingatia ukweli, uwazi pamoja na uwajibikaji katika kutekeleza majukumu mbalimbali yanayohusu soka nchini umekuwa ni kichocheo kikubwa kwa wadhamini kujitokeza na kuwekeza kwenye ligi. Aidha alienda mbali zaidi akisema kuwa uwekezaji huo utainua kiwango cha soka hapa Tanzania na pia utazidi kuleta sifa kwa taifa.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo Rais wa TFF Wallace Karia alisema tukio hilo la kusaini mkataba na Benki ya NBC ni mwendelezo wa TFF kuwashirikisha wadau mbalimbali kuwekeza katika mpira wa miguu na hivyo kusaidia na kurahisisha gharama za uendeshaji ikiwa ni pamoja na kuviwezesha vilabu vya ligi kuu kushiriki michezo ya ligi bila kuwa na changamoto kama vile za usafiri,ukosefu wa vifaa bora vya michezo,viwanja vilivyo chini ya kiwango na mengine mengi.
Karia aliendelea kusisitiza kwamba wakati anaingia madarakani mwaka 2017 moja ya kipaumbele chake (First Eleven of Karia) ilikuwa ni kuboresha ligi zote ikiwemo Ligi Kuu, hivyo anafurahi kuona jambo hilo limetimia kwa kiasi kikubwa ambapo hivi sasa Ligi Kuu Tanzania Bara inashikilia nafasi ya nane (8) kwa ubora barani Africa, hivyo basi mkazo zaidi utaendelea kuwekwa katika kuwashirikisha wadau mbalimbali nchini na hata nje ya nchi kuwekeza katika soka letu na kusaidia ligi ya Tanzania kukua na kupanda zaidi katika nafasi za juu barani Africa.
Ligi kuu Tanzania Bara kwa msimu wa 2021/2022 itajulikana kwa jina la NBC-Tanzania premier League, ligi hiyo ilianza kutimua vumbi mnamo Septemba 27,2021 huku mizunguko miwili ikiwa tayari imekamilika na timu shiriki kwenda kwenye mapumziko kupisha ratiba ya michezo ya kimataifa kuendelea.