Timu ya Taifa chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes itacheza mechi zake mbili za hatua ya Makundi michuano ya CECAFA U20 inayoanza Jumamosi hii nchini Uganda majira ya saa saba mchana badala ya saa 10 jioni kama ratiba ya awali ilivyokuwa ikionyesha.

Mabadiliko hayo yamefanywa na Baraza la Vyama Vya Soka na Vilabu Afrika Mashariki na Kati, CECAFA ambapo sasa Tanzania itacheza dhidi ya Ethiopia Jumapili saa saba mchana, k na mchezo dhidi ya Kenya Jumanne mchana kabla ya kufunga dimba na Zanzibar Alhamisi saa 10 jioni.

Kocha wa Ngorongoro Heroes, Zuberi Katwila amesema ameanza kuwaandaa vijana wake kucheza muda huo wa mchana na tayari wameonyesha mwelekeo jambo ambalo linampa Imani kuwa watafanya vizuri.

“Ni changamoto kubwa kucheza kwenye jua kali hasa ikizingatiwa kuwa uwanja wenyewe ni wa nyasi bandia, lakini tumefanya mazoezi majira hayo ya mchana kwa leo Ijumaa na kesho tutafanya tena ili kuzoea,” amesema Katwila.

Kwa upande wake kiungo wa timu hiyo, Gustapha Saimon amesema wamejiandaa vyema kukabiliana na mabadiliko hayo kwani lengo lao kubwa ni kuhakikisha wanaipeperusha vyema bendera ya Tanzania katika mashindano hayo.

“Lengo letu kama wachezaji ni kufanya vizuri katika mashindano haya. Tunaitazama hii kama fursa ya kujiuza Zaidi hivyo tutaendelea kujituma ili kuweza kufanya vizuri,” amesema Gustapha

Ngorongoro imefanya mazoezi yake leo mchana katika Uwanja wa Kituo Cha Ufundi cha FUFA mjini Jinja ili kujiweka sawa kabla ya kutupa karata yake ya kwanza Jumapili.