JULIO: “Ngorongoro Heroes Tuko Imara Tunakwenda Kushindana na Sio Kushiriki”

Kocha wa timu ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (U20) Tanzania “Ngorongoro Heroes” Jamhuri Kihwelo ameongea na waandishi wa habari  Februari 1, 2021 katika ukumbi wa mikutano wa TFF juu ya maadalizi  ya timu kuelekea katika fainali za AFCON zitakazo fanyika huko nchini Maurtania.

Jamhuri amesema kwamba kikosi chake kipo timamu na kimejiandaa vizuri tayari kwa mashindano hayo na anaamini watapata matokeo yaliyo mazuri, kwani vijana hao walipata muda wa kufanya mazoezi ya kutosha toka walipopiga kambi huko Arusha katika hoteli ya Ngurudoto kwa muda wa siku kumi na baadaye kuhamia jijini Dar es salaam katika hoteli ya Tiffany ambako huko nako bado wanaendelea kujinoa vilivyo tayari kukabiliana na michuano hiyo.

Kocha huyo aliendelea kusisitiza kuwa licha ya kwamba hiyo ni mara ya kwanza kwa timu ya Taifa ya U20  kupata nafasi ya kushiriki katika mashindano makubwa kama hayo, bado sio jambo linalomtisha kwani anaamini katika uwezo wake na uwezo wa kikosi chake pia.

Zaidi ya hayo aliushukuru uongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF kwa juhudi kubwa wanazozifanya katika kuhakikisha timu hizi za vijana zinazidi kufanya vizuri ndani na nje ya nchi; kwani msingi wa kupata timu bora ya taifa  ni kuanza kuwatengeneza na kuendeleza vipaji vichanga jambo amblo TFF inalisimamia na kuletekeleza kwa nguvu zote.

Hata hivyo, kocha huyo hakusita kutoa neno kwa watanzania wanaozibeza timu za taifa au wachezaji wanaochaguliwa na makocha kuunda timu hizo na kuwataka kuacha kufanya hivyo na badala yake waziunge mkono na kuziombea mema timu hizo ambazo zinafanya kazi kubwa ya kuliwakilisha taifa. Julio “alisema linapokuja suala la timu za taifa basi utaifa na uzalendo unaanza kwanza kabla ya mambo mengine na endapo watanzania wote tukiwa kitu kimoja katika kuzisaidia na kuzipa hamasa timu za taifa hakika zitaendelea kufanya vizuri na kuipeperusha bendera ya Tanzania duniani kote”.

Michuano hiyo ya fainali za Afcon kwa timu za under 20 inatarajiwa kuanza kurindima Februari 14, 2021 huko nchini Maurtania ambapo timu ya Tanzania ipo katika kundi C linalojumuisha timu za  Ghana, Gambia na Morocco.