Baada ya kupata ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Ethiopia kwenye mechi ya ufunguzi ya Michuano ya CECAFA U20 Challenge Cup inayoendelea mjini Jinja, Uganda, Timu ya Taifa ya Tanzania U20, Ngorongoro Heroes imeendelea kujifua kujiweka sawa kwa mechi ya pili dhidi ya Kenya itakayochezwa kesho Jumanne saa 7;00 mchana.

Mechi hiyo inatarajiwa kuwa kali na ya aina yake hasa baada ya Kenya kuifunga Zanzibar mabao 5-0 katika mechi ya ufunguzi iliyochezwa jana Jumapili jioni kwenye Uwanja wa Kituo cha Ufundi cha Fufa,Jinja.

Kocha Mkuu wa Ngorongoro Heroes, Zuberi Katwila amesema kwa namna alivyoitazama Kenya wanatakiwa kufanya kazi kubwa ili kuweza kupata ushindi wa pili na kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

“Tumewaona Kenya, ni timu nzuri. Uzuri ni kwamba hata wachezaji wetu pia walikuwepo uwanjani na kuona wapinzani wetu wamefanya kitu gani,Utakuwa ni mchezo mzuri na wa ushindani, tuna imani timu yetu itafanya vizuri,” amesema Katwila.

Kwa upande wake beki wa kati wa timu hiyo, Oscar Masai, amesema tayari mwalimu wao amewapa mbinu sahihi za kuikabili Kenya hapo kesho, huku akisema wamejipanga kushindana.

Naye straika wa timu hiyo, Andrew Simchimba aliyefunga mabao matatu ‘Hat Trick’ kwenye mechi dhidi ya Ethiopia, amesema anatamani kuendelea na kiwango chake bora alichoanza nacho katika mashindano hayo ili kuweza kuisaidia timu.