Nusu Fainali CECAFA Kupigwa Agosti 24,2022
Michezo ya hatua ya nusu fainali michuano ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika kwa wanawake ukanda wa CECAFA inayoendelea hapa nchini inatarajiwa kupigwa Agosti 24, 2022 kwa timu mbili kutoka kundi A kukiwasha na timu mbili kutoka kundi B.
Hatua hiyo ya nusu fainali itakwenda kupigwa mara baada ya timu shiriki takribani 8 kumalizana kwenye makundi, ambapo kinara wa kundi B Simba Queens FC rasmi sasa kukipiga dhidi ya timu ya Rwanda AS Kigali WFC ambayo imeshika nafasi ya pili kwenye kundi A.
Wakati CBE FC vinara wa kundi A kutoka Ethiopia wakiwa na rekodi ya kutopoteza mchezo wowote kwenye hatua ya makundi sawa kabisa na Simba Queens FC ambao pia hawajapoteza mchezo kwenye hatua hiyo wenyewe watakwenda kukutana na timu ya SHE Corporates ya Uganda ambayo imemaliza kwenye nafasi ya pili kundi B.
Hata hivyo CBE FC ndio timu pekee inayoongoza kwa idadi kubwa ya magoli, CBE FC imefunga jumla ya magoli 16 kwenye hatua ya makundi, huku Loza Abera Geinore nahodha wa kikosi hiko akiwa na jumla ya magoli 9.
Mpaka sasa nyota huyo wa CBE FC ndiye anashikilia rekodi ya kufunga magoli mengi zaidi kwenye michuano hiyo kwa mwaka huu.
Licha ya timu hizo 4 kwenda kutupa karata zao kwenye hatua inayofuata, zile nyingine Fofila PF ya Burundi, Warriors Queens FC ya Zanzibar, Garde Republicaine FC na Y.J. Stars FC kutoka Sudani Kusini zikifungasha virago baada ya hatma yao kwenye michuano.