Young Africans na  Polisi Tanzania Hakuna Mbabe Amri Abeid Arusha

Mabingwa wa kihistoria Dar Young Africans wameshindwa kuvuna alama tatu katika mchezo uliochezwa kati yao na timu ya Polisi Tanzania ambapo mchezo huo ulimalizika kwa sare ya bao1-1.

Mchezo  huo uliopigwa majira ya saa 10:00 jioni katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid uliopo jijini Arusha ulikuwa na umuhimu kwa pande zote mbili ambapo endapo Young Africans wanegefanikiwa kushinda basi wangeliweza kurudisha hamasa kwa mashabiki wao na pia kufikisha alama 52 na hivyo kujiweka katika nafasi nzuri za ubingwa. Hali kadhalika Polisi Tanzania nao wangeweza kusogea kwenye nafasi nzuri zaidi endapo wangefanikiwa kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo.

Mchezo ulikuwa mgumu kwa pande zote mbili licha ya timu ya Young Africans kufanikiwa kupata bao la kuongoza katika dakika ya 44 kipindi cha kwanza, bao hilo likifungwa na mchezaji Nyota kutoka Burundi Fiston  Abdulrazack  aliyeunganisha kwa kisigino pasi safi iliyopigwa na Mshambuliaji kutoka Congo Tuisila Kisinda; bao hilo lilidumu mpaka kipindi cha kwanza kinakamilika.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kwa pande zote mbili; Polisi Tanzania wakitaka kusawazisha wakati Young Africans nao wakitaka kuongeza bao la pili ili kujihakikishia ushindi kwenye mchezo huo jambo ambalo halikuwezekana kwa upande wa Young Africans.

Baada ya mchezo huo kuwa mgumu, makocha wote waliamua kufanya mabadiliko ambapo kocha wa Young Africans Cedric Kaze alimtoa Ditram Nchimbi(JZ 02) na kumuingiza Deus David Kaseke (JZ 27); mabadiliko hayo yalifanyika kunako dakika ya 18 ya kipindi cha pili wakati kocha wa Polisi Tanzania Malale Hamsin, naye akimtoa Marcel Kaheza(JZ10) na kumuingiza Gerald Mathias (JZ 30) dakika ya 55. Huku kwenye dakika hiyo hiyo.

Katika dakika ya 78 kipindi cha pili kocha Malale alimtoa Kassim Shaban akimpisha Pius Buswita(JZ 03).  Wakati Kaze  naye akimtoa Haruna Niyonzima (JZ 08) na kumuingiza Zawadi Mauya (20) mnamo dakika ya 78  kabla ya kumtoa Kibwana Shomari kwenye dakika za majeruhi na kumuingiza Wazir Junior (JZ 16).

Kuingia kwa wachezaji wote hao hakukuwa na faida kwa upande wa kikosi cha Young Africans kwani waliweza kuruhusu bao la jioni huku Polisi Tanzania wakiwa pungufu baada ya Kelvin Yodani kutolewa kwa kadi nyekundu manamo dakika ya 89 ya mchezo huo kutokana na kumchezea madhambi Fiston Abdulrack kwa mara ya pili baada ya kumchezea hivyo awali alipozawadiwa pia kadi ya manjano. Hata hivyo, kutoka kwa Yondani hakukuwazuia Polisi Tanzania kusawazisha bao katika dakika za jioni kabisa na kuufanya mchezo huo kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Kocha Cedric Kaze wa Young Africans alisema kuwa mchezo huo ulikuwa ni mgumu na katika kipindi cha pili wachezaji wake walionekana kupoteza umakini na hivyo kushindwa kulinda bao lao katika dakika za mwishoni kabisa kitu ambacho kiliwagharimu na kufanya matokeo kuwa kama yalivyo. Mbali na hayo, kocha Kaze hakusita kuendelea kuwatia moyo  wachezaji wake kwa kuwambia kuwa wazidi kupambana zaidi ili kuweza kutwaa ubingwa kwani ligi bado ni ngumu na kwamba lolote linaweza tokea.

Wakati hayo yakisemwa na kocha wa Young Africans;  kocha wa Polisi Tanzania Malale Hamsin yeye aliwapongeza wachezaji wake kwa kupambana mpaka dakika ya mwisho na hatimaye kufanikiwa kusawazisha bao hilo, kitu ambacho hakikuwa chepesi kwani alijua wazi kuwa timu aliyokutana nayo ilikuwa imetoka kupoteza mchezo wake dhidi ya Coastal Union ya Tnaga, na hivyo ilikuwa inapambana kujiweka katika nafasi nzuri kwenye mbio za ubingwa. Kuhusu mabadiliko aliyoyafanya alidai kuwa alipokwenda kwenye mapumziko aligundua makosa ya wapinzani wake na hivyo akatoa maelekezo kwa kikosi chake; jambo lililompa matokeo chanya baada ya kumuingiza mfungaji wa bao, Pius Buswita.

Kwa matokeo hayo, timu ya Young Africans inafikisha alama 50 ikiwa mbele ya watani wao Simba kwa michezo minne; Simba ambao mpaka sasa wana alama 45, baada ya kushuka dimbani mara 19. Matokeo hayo ya Young Africans yanazidi kuipunguza matumaini timu hiyo katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2020/2021; ubingwa  ambao imeukosa kwa miaka mitatu mtawalia.