Rais Samia Awapongeza Twiga Stars Kubeba Kombe Afrika Kusini

Rais wa Jumhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amsema kuwa timu ya Taifa ya Twiga Stars imeendelea kuijengea heshma Tanzania baada ya kufanikiwa kubeba Kombe kwenye mashindano ya COSAFA Women’s Championship 2021 yaliyokuwa yanafanyika nchini Afrika ya Kusini tangu 29 Septemba hadi 09 Oktoba, 2021 huku ikiwa na historia ya kufanya vizuri kwenye mashindano mengi iliyofanikiwa kwenda kushiriki.

Mhe. Rais Samia aliyasema hayo Oktoba 10, 2021 alipokuwa analihutubia Taifa kwenye Mkutano wa Uzinduzi wa Kampeni ya Maendeleo uliowakutanisha viongozi, wananchi na wadau mbalimbali wa siasa na maendeleo nchini katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya uliopo Jijini Dodoma.

Akitoa pongezi kwa kikosi cha Twiga Stars Mhe. Rais Samia alieleza kuwa timu za wanawake zimekuwa zikishiriki katika mashindano tofauti tofauti huku zikifanikiwa kurejea na vikombe vingi nchini na hivyo kuliletea sifa kubwa Taifa.

Aidha, Mhe. Samia alitanabaisha kuwa kwa kumbukumbu aliyonayo hadi sasa timu za mpira wa miguu za wanawake Twiga Stars, Tanzanite (U20) pamoja na U17 zimefanikiwa kutwaa vikombe vya kimataifa takribani vitano pale zinapokwenda kuiwakilisha nchi.

Rais Samia hakuishia kuipongeza Twigar Stars pekee, bali pia benchi zima la ufundi lililoko Afrika Kusini pamoja na uongozi wote wa TFF ukiongozwa na Rais Wallace Karia, kwa usimamizi mzuri wanaoufanya kwa timu za Taifa.

Mbali na maelezo hayo ya pongezi, Mhe. Rais alisema kuwa anatambua uwepo wa Twiga Stars na Timu nyingine za wanawake zinazofanya vizuri; kisha akamezea moyoni kuhusu nini anakusudia kukifanya kwa timu hizo za wanawake ambazo zimekuwa zikiendelea kuliletea sifa kemu kemu taifa la Tanzania.

Kabla ya kauli hiyo Rais Samia aliandika kwenye ukurasa wake wa twita mara tu baada ya timu hiyo kutwaa ubingwa wa mashindano hayo ya ‘COSAFA Women’s Championship 2021’yaliyofikia tamati Oktoba 09, 2021 nchini Afrika Kusini na Tanzania kuibuka mabingwa wapya baada ya kuifunga Malawi kwa bao moja kwa sifuri; bao hilo likifungwa na Enekia Kasongo Lunyamila(17) dakika 53  ya fainali hiyo na kudumu mapaka mwisho wa mchezo.

Tanzania ilikwenda kushiriki ikiwa ni nchi mualikwa ikiwakilisha Ukanda wa CECAFA; mbali na kombe hilo, makombe mengine ambayo Tanzania imewahi kushinda kwenye michuano mbalimbali ya kimataifa ya wanawake ni pamoja na; COSAFA U17 WOMEN’S CHAMPIONS (2020); COSAFA U20 WOMEN’S CHAMPIONS (2019); CECAFA WOMEN’S CHAMPIONS (2018); CECAFA WOMEN’S CHAMPIONS (2016) huku ikifanikiwa pia kufika kucheza katika hatua ya fainali, nusu na robo fainali kwenye michuano mbalimbali ya kimataifa.

Timu hiyo ya Twiga Stars inatarajiwa kurejea nchini kwa ajili ya maandalizi ya Michuano ya kufuzu AFCON inayotarajiwa kuanza mwezi Oktoba, mwaka huu (2021).