Prisons Yashindwa Kutamba Nyumbani

Timu ya Tanzania Prisons imeshindwa kutamva mbele ya Coastal Union (Wagosi wa Kaya) baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliopigwa Novemba 10, 2022 majira ya saa 10:00 jioni kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Mchezo huo uliokuwa wa kiporo kwa upande wa Wagosi wa Kaya ulikuwa na ushindani kiasi licha ya Wajelajela hao kushindwa kuonesha ubora walionao ukilinganisha na michezo kadhaa waliyocheza.

Ni dakika 4 tu za mchezo huo ziliitosha Coastal Union kuweza kuandika bao la kuongoza bao lililofungwa na mchezaji Mabaad Maulid, huku bao la pili likikomelewa na Hammad Majimengi dakika ya 60. Mabao hayo mawili yalitosha kuinyong’onyeza Prisons ambayo licha ya kufanya mabadiliko kadhaa bado haikuweza kubadili ubao wa matokeo mpaka dakika 90 zinakamilika.

Kocha wa Prisons Patrick Odhiambo alisema kuwa wachezaji wake hawakuwa katika kiwango bora akiongeza kuwa kusekana kwa baadhi ya nyota wake pia kulichangia kutopata matokeo mazuri katika mchezo huo. Hata hivyo, Odhiambo aliseam ligi bado watajitahidi kufanyia kazi makosa yote na kutia morali wachezaji ili waweze kujutuma zaidi uwanjani kwa ajili ya kuhakikisha timu inapata matokeo na kuendelea kukaa kwenye nafasi nzuri katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Msimu huu wa 2022/2023.

Kwa upande wake Yusuph Chipo, kocha wa Wagosi wa Kaya alisema matokeo waljoyapata wao yalitokana na kupata muda mwingi wa kumpunzika lakini pia kuutumia vema muda huo walioupata kujifua kwa ajili ya kupata matokeo. Na kwamba wachezaji wake waliingia kwenye mchezo wakiwa na ari na morali ya hali ya juu ya kusaka matokeo tu na si vinginevyo.

Alisema baada ya kugundua udhaifu wa Prisons mwenye mchezo huo basi akaongea na wachezaji wake kutumia vyema upenyo huo ili kujipatia matokeo waliyoyakusudia ili kuanza kukaa pazuri zaidi.

Matokeo ya mchezo huo kati ya Tanzania Prisons na Coastal Union yameifanya Coastal Union kusogea juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC kutoka nafasi ya 13 hadi 11 huku ikifikisha alama 11baada ya kushuka dimbani mara 8 wakati Prisons wao wakisalia kwenye nafasi yao ya 8 baada ya kucheza michezo 11 na kukusanya alama 14.