Rais Dkt. Samia Azipongeza Simba na Young Africans Kimataifa

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan amezimwagia sifa timu za Simba na Young Africans zinazoshiriki michuano ya Kimataifa ya CAF kwa kutumia vyema fursa aliyotoa kwa vilabu hivyo kufuatia ahadi ya kununua kila goli moja litakalofungwa kwenye michuano hiyo kwa kiasi cha TSh. Milioni Tano (5,000,000).

Rais Samia aliyasema hayo alipokuwa akihutubia kwenye sherehe ya kutimiza Miaka Miwili ya Uongozi wake zilizoandaliwa na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) na kufanyika kwenye uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam, Jumapili ya Machi 19, 2023.

Akitoa pongezi hizo kwa timu kongowe nchini, zinazowakilisha kwenye Michuano ya Kimataifa inayosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) Dkt. Samia alisema kuwa wachezaji na viongozi wa timu hizo wanafanya kazi nzuri ya kulitangaza Taifa la Tanzania katika medani ya Soka, na kwamba yeye yupo tayari kuendelea kutimiza ahadi yake aliyoitoa bila shaka.

Alisisitiza na kuwaondoa shaka wachezaji, wadau na mashabiki wa timu hizo, kuwa fedha bado ipo haijaisha na haiwezi kuisha huku akivitaka vilabu hivyo kuongeza juhudi zaidi ya kupachika mabao wavuni katika michuano hiyo ili kuhakikisha zinaendelea kuutumia fursa hiyo vyema zaidi ikiwa ni pamoja na kutimiza malengo yao. Alisema timu hizo zinapaswa kuendelea kuwa na hamu ya kufunga hivyo hivyo hata pale ambapo fedha hizo zitakapokoma kutolewa huko mbeleni.

” Nilisikia na kuona kwenye mitandao ya kijamii watu wanasema Simba imemaliza fedha za Mama baada ya kushinda bao 7-0 dhidi ya Horoya na kuvuna TSh. Milioni Thelathini na Tano Kwa mechi moja, ambapo ukijumuisha na yale mabao mawili wanakuwa wamepata 45 milioni. Wakati Young Africans nao wakiwa wameisha jikusanyia Milioni Thelathini; fedha bado ipo, waongeze juhudi tu,”  alisema Rais Samia na kuongeza kuwa: ” atafurahi zaidi endapo timu hizo zitaendelea kushinda hivyo hivyo  hata kama fedha zitakuwa hazitolewi.”

Aidha, Rais Samia amewataka wachezaji wa timu hizo kuendelea kujituma zaidi kwani mpira ndiyo ajira na kwamba kadri wanavyozidi kusonga mbele kwenye hatua mbalimbali ndivyo ambavyo nchi inazidi kupata Sifa njema kisoka Duniani.

Mbali na hayo, Rais Samia ameahidi kuendelea kuboresha na kuimarisha michezo kama ambavyo Serikali ya Awamu ya Sita ilivyokwisha kujipambanua katika kusapoti michezo yote ikiwa ni pamoja na Mpira wa Miguu; kuwani mchezo huo unaajiri vijana wengi zaidi nchini.

Timu za Simba na Young Africans zinapambana ili kufuzu hatua ya robo fainali; Simba inashiriki Mashindano ya Klabu Bingwa Afrika huku Young Africans wao wakifanya hivyo  kuitaka hatua hiyo kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.