Want create site? Find Free WordPress Themes and plugins.

Rais Karia Afungua Rasmi Kozi ya Ukufunzi Ngazi ya CAF

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania(TFF) Wallace Karia amefungua rasmi kozi ya ukufunzi ngazi ya CAF Septemba 07, 2021  inayofanyika katika Makao Makuu ya Shirikisho hilo yaliyopo  Ilala jijini  Dar es salaam, ikijumuisha washiriki wapatao 11 kutoka Mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Visiwani.

Kozi hiyo ya siku 10  ina lengo la  kuzidi kuwajengea uwezo  waalimu hao wa Mpira wa miguu  ili waweze kufanya kazi yao kwa umakini na ueledi, lakini pia kuongeza idadi ya wakufunzi wa ndani ambao watakuwa na sifa  za kufundisha  mpira wa miguu kwa viwango vinavokubalika kimataifa.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kozi hiyo Rais Karia alisema, anafurahishwa kuona jinsi waalimu walivokuwa na hamasa  kubwa ya kupenda kujifunza vitu vipya katika mchezo wa mpira; kwani tasnia hiyo imendelea kukua na mambo mengi yanaongezeka  kila kukicha hivyo kuongeza ujuzi ni jambo la lazima kwa waalimu wa mpira ili waweze kuendana na kasi ya mabadiliko hayo.

Akiongea kwa msisitizo Karia alitoa rai kwa wakufunzi wa kike kuendelea kujitokeza kwa wingi na kuchangamkia fursa  pindi kozi hizi zinapotangazwa ili pawepo na usawa  wa kijinsia katika tasnia hiyo na siyo kuwaachia wanaume peke yao .

Mbali na hayo aliongeza kwamba  katika kipindi cha uongozi wake kozi hizi zitakuwa na mwendelezo na atahakikisha zinatolewa mara kwa mara katika ngazi zote akianza na ngazi ya mikoa huku akitolea mfano wa kozi  za Grass roots zinazoendelea kutolewa na kusema kwamba kwa siku za usoni kozi hiyo itatolewa  visiwani Zanzibar.

Naye Mkurugenzi wa ufundi Oscar Mirambo alisema kozi hiyo italeta matokeo chanya si  tu kwa Tanzania bali Afrika kwa ujumla; kwani washiriki hao watakwenda kutatua changamoto mbalimbali zilizopo kwa waalimu wa mpira  na kutengeneza wachezaji walio bora ambao watakuwa na uwezo wa kufanya vizuri  katika mashindano yote watakayoshiriki.

Kwa upande wa mkufuzi wa kozi hiyo mwalimu  Honor Janza ( Elite CAF Instuctor) yeye alisema anashukuru  kwa mapokezi mazuri aliyoyapata kutoka kwa uongozi wa TFF lakini pia kwa shirikisho la mpira wa miguu barani Africa (CAF) kwa kumwamini kufundisha walimu wa mpira wa miguu nchini Tanzania hivyo atatoa elimu stahiki anayoamini kwamba itazalisha makocha wengi wenye ujuzi sahihi na watakaosimamia misingi ya kada yao vile inavyotakiwa  ili hapo baadaye Tanzania iweze kuzalisha timu bora na waalimu wenye viwango bora watakaoweza kujiendesha bila kutengemea waalimu kutoka nje.

Kozi hiyo  ya ukufunzi ngazi ya CAF ni mara ya kwanza kutolewa hapa nchini Tanzania Ikiwa ni moja ya mpango wa idara ya ufundi kupitia kitengo cha elimu (coach education) kuendelea kuwajengea uwezo wakufunzi wa ndani ili kuleta mabaliko chanya katika mchezo wa mpira wa miguu.

 

 

Did you find apk for android? You can find new Free Android Games and apps.