Rais Karia Asisitiza Umoja na Mshikamano kwa Wakufunzi wa Ukocha

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF Wallace Karia amewataka washiriki wa kozi ya Ukufunzi wa Ukocha Ngazi ya FIFA kwenda kushirikiana vyema na viongozi wa vyama vya Soka Mikoani pamoja na viongozi wa taasisi na Serikali, akidai kufanya hivyo kutaongeza maelewano baina yao jambo ambalo litaimarisha mawasiliano na ushirikiano mzuri katika kuendeleza soka nchini.

Hayo aliyasema Novemba 16, 2021 alipokuwa akifungua Kozi hiyo ya Ukufunzi daraja ‘A’ ngazi ya FIFA kwenye ukumbi wa mikutano uliopo Makao Makuu ya TFF Karume Ilala Dar es Salaam. Rais Karia alieleza kuwa suala la kupata mafunzo ni moja na kuyafanyia kazi mafunzo hayo ni jambo jingine ambalo linahitaji ushirikiano na ufanyaji kazi wa pamoja ili elimu hiyo iweze kuleta tija.

Aidha, Rais Karia aliongeza kuwa kumekuwa na kozi nyingi zikitolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania kwa kushirikiana na FIFA, na CAF, lakini washiriki wamekuwa wakishindwa kujitokeza kwa wingi na wale wachache wanaopata elimu hiyo bado nao hawaendi kuifanyia kazi ipaswavyo wakati huo huo na baadhi ya hao wachache wamekuwa wakiibua migogoro isiyo na tija katika maeneo yao ya kazi. Mambo hayo yanapelekea kurudisha nyuma juhudi zinazofanywa na TFF za kutaka kuendeleza soka la Tanzania.

Akahitimisha kwa kuwashukuru wakufunzi na washiriki wote wa kozi hiyo huku akiwaomba wakufunzi kuendelea kujitoa kuja kutoa mafunzo hayo kwa ajili ya kuendeleza soka la Tanzania kwani hilo ndilo dhumuni anuai la TFF kuufanya mpira wa Tanzania kuweza kukua zaidi. Alisema kuwa huwezi zungumzia kukua kwa mpira pasipo kutoa elimu kwa wakufunzi wa makocha na makocha wenyewe kwani wao ndio hutengeneza wachezaji wenye viwango bora vitakavyotutambulisha kimataifa.

Naye mkufunzi wa kozi hiyo Mokata Frans Mogashoa kutoka Afrika Kusini alisema anafurahishwa na ushirikiano anaoupata kutoka kwa washiriki kwani wamekuwa wasikivu na wenye utayari kutaka kujifunza jambo ambalo linawapa moyo wakufunzi kuendelea kutoa mafunzo hayo.

Akifafanua zaidi kuhusu kozi hiyo, Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF Oscar Mirambo alisema kuwa lengo na dhumuni kuu la kozi hiyo ni kuwaongezea uwezo zaidi wakufunzi wa ukocha ili kuweza kukidhi mahitaji ya wakati uliopo. Hivyo, yeye akiwa miongoni mwa washiriki waandamizi wa kozi alisema kuwa anafarijika pia kuona muamko na ari ya kujifunza jambo ambalo linatia moyo.

Kozi hiyo ya Ukufunzi wa Ukocha imejumuisha washiriki kumi na tano (15) ikiwa ni pamoja na wakufunzi waandamizi. Washiriki hao ni pamoja na Alfred Alexander Itaeli, Abdul mwingange, Fikiri Mahiza, Wane Mkisi, Samson Mzee Mkisi, Cyprian Maro, Juma Mwambusi, Mohamed Tajdin Hamour Janza , Martin Hammel, Luhanja Makunja, Nasra J. Mohammed na Rogasian Kaijage.