Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania Wallace Karia amewapongeza wachezaji na benchi la ufundi la timu ya Taifa ya wasichana  wenye umri chini ya miaka 17 kwa kutwaa ubingwa wa COSAFA baada ya kuwaondosha Zambia kwa penati 4-3 katika mchezo wa fanali uliochezwa siku ya Juma mosi tarehe 14 Novemba,2020 nchini Afrika Kusini.

Hayo aliyasema usiku wa Jumapili ya tarehe 15 Novemba, 2020 katika uwanja wa Mwalimu Julius K. Nyerere alipowaongoza wafanyakazi wa TFF na wadau mbalimbali wa soka kwenda kuipokea timu hiyo ya wanawake U17 baada ya timu hiyo kuleta kikombe cha COSAFA.

Akizungumza na waandishi wa habari waliokuwepo uwanjani hapo, Rais Karia alisema kuwa timu hiyo imejitahidi kutimiza yale yote aliyowahimiza kufanya siku alipokuwa akiziaga timu hizo mbili; yaani Twiga Stars na hiyo ya U17 ambapo aliwaaga kwa kusema angekuwa na furaha endapo timu mojawapo ingefanikiwa kurudi na kikombe. Kwa kufanikiwa kwa timu hiyo kurejea na kikombe hicho ni kutimiza kiu aliyokuwa nayo.

Aliendelea kutanabaisha kwamba huo ni muendelezo tu wa mafanikio ambayo timu za Taifa zimekuwa zikiyapata na kuwafanya TFF ambao ndio wasimamizi wakuu wa timu zote za Taifa kutembea kifua mbele kufuatia mafanikio ambayo yamekuwa yakiletwa na timu hizo.

Aidha Rais aliongeza kuwa soka la wanawake limekuwa na mvuto wa aina yake na hivi sasa idadi ya mashabiki inazidi kuongezeka siku hadi siku kutokana na timu hizi kuendelea kufanya vizuri zaidi ukilinganisha na timu za wanaume. Alisema kuwa hayo ndiyo matunda ya kuwekeza zaidi katika soka la wanawake ambapo TFF hivi sasa imezidi kujikita katika kuwaongezea uwezo zaidi wanawake katika masuala yote yanayohusiana na mpira wa miguu pamoja na uongozi ili wazidi kujiamini zaidi na waweze kushindana katika tasnia hii ya michezo inayozidi kubadilika na kukua kila uchao.

Hata hivo, Rais Karia alitoa pongezi za dhati kwa  Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mheshimiwa Rais John Joseph Pombe Magufuli na Makamu wake Mama Samia Suluhu ambaye ndiye mlezi wa Timu za taifa za wanawake kwa ushindi wa kishindo walioupata kuiongoza nchi ya Tanzania kwa awamu ya pili, hivyo basi ujio wa kombe hilo ni njia mojawapo ya kuwapongeza viongozi hao kwa ushindi huo. Mwisho Rais Karia akaiomba serikali kuendelea kutoa ushirikiano kwa programu zote za vijana kwa wanaume na wanawake kwani ndio msingi utakaojenga timu bora za Taifa kwa miaka ijayo.

Tukio hilo la mapokezi ya mabingwa hao wa COSAFA kwa mwaka huu wa 2020 (timu ya U17) wasichana yalihudhuriwa na Makamu wa pili wa Rais ndugu, Steven Mnguto, katibu Mkuu wa TFF ndugu, Kidao Wilfred, Mkurugenzi wa ufundi TFF ndugu, Oscar Mirambo, Makamu mwenyekiti wa soka la Wanawake Bi. Rose Kisiwa pamoja na baadhi ya wafanyakazi  wa TFF na wadau wengine wa soka.