Want create site? Find Free WordPress Themes and plugins.

Rais Karia  Kuishika Mkono Mwanga

Rais wa Shirirkisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF Wallec Karia anayeendelea na ziara zake za kikazi kutazama shughuli mbalimbali za maendeleo ya mpira wa miguu hapa nchini ameahidi kuunga juhudi zinazofanywa na wadau wa soka wilayani Mwanga mkoa wa Kilimanjaro.

Rais Karia amezungumza hayo Disemba 13, 202 alipokuwa anakagua baadhi ya miundombinu ya viwanja katika wilaya ya Mwanga, akieleza kuwa Shirikisho lipo tayari kushirikiana na wadau  pamoja na viongozi wa wilaya ya Mwanga kwa kutoa mafunzo mbalimbali sambamba na ushauri wa kitaalam kuhakikisha unajengwa uwanja wa kisasa.

Mbali na hayo Rais ameeleza kuwa Shirikisho litawapatia mafunzo ya kozi mbalimbali ikiwemo Grassroot na kozi nyingine za ukocha na utawala kwenye mpira wa miguu ilikuhakikisha maendeleo yanapatikana wilayani humo akionesha imani kubwa kufikia malengo kutokana na mwanzo mzuri alioukuta wilayani hapo.

Aidha Rais Karia aliweka wazi kuwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania lipo katika hatua za kukarabati viwanja ambavyo vipo katika hali chakavu ili kukuza mchezo wa soka na akitaka wilaya ya Mwanga kuwa mfano kwa maeneo mengine.

Naye mbunge wa jimbo la Mwanga Joseph Thadeyo amesema kuwa lengo hasa la wao kumualika Rais Karia  ni kutafuta kuomba ushauri na maelekezo ili kuhakikisha wilaya hiyo inaendana na kauli ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan “TUMEFUNGUA NCHI YETU NA KUJENGA UCHUMI”.

Mbunge huyo aliongeza kuwa lengo lake ni kuifanya Mwanga kuwa ni sehemu ambayo kutakuwa ni moja kati ya mahala ambapo kutakuwa ndio kitovu cha kupatikana vijana wenye vipaji, walimu wa mpira wenye weredi lakini pia viwanja vinavyokidhi mahitaji ya mashindano tofauti tofauti.

Ikumbukwe kwenye ziara hiyo  Rais Karia alitembelea  kituo cha soka cha Moskisa kuangalia maendeleo ya vijana wanaofundishwa mpira wa miguu, pia  alifanya kikao na Mkuu wa Wilaya hiyo Abdallah Mwaipaja na Mbunge wa jimbo hilo Joseph Thadeyo.

Did you find apk for android? You can find new Free Android Games and apps.