Rais Samia aahidi kutoa  tiketi 2000 kwa mashabiki wa Taifa Stars

Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameahidi kutoa tiketi 2000 kwa mashabiki wa Taifa Stars kwa ajili ya kwenda kushuhudia mchezo wa marudiano  wa kufuzu AFCON Kati ya Taifa Stars  dhidi ya Uganda utakaopigwa katika uwanja wa Benjamin Mkapa  Machi 28,2023.

Mheshimiwa Rais Ametoa ahadi hiyo kupitia kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa  katika mkutano na wanahabari ulioandaliwa na TFF  uliobeba jina la ‘Jambo la nchi’ uliofanyika katika hoteli ya Tiffany Diamond  jijini Dar es Salaam.

Akiongea kwa njia ya simu Mheshimiwa Waziri mkuu alisema “ni fursa kubwa ambayo tutaipata endapo timu yetu itafuzu  kushiriki AFCON kwasababu hadhi ya taifa letu itapanda  lakini pia tutapanda katika viwango vya soka Duniani. Kwa kutambua umuhimu huo Rais  ameniagiza niseme kuwa atatoa tiketi 2000 kwa ajili ya mashabiki kwenda kutazama mechi ya marudiano itakayochezwa hapa nyumbani”.

Mbali na kuwasilisha ujumbe wa Rais Samia, Waziri Mkuu aliongeza tiketi 2000 kwa ajili ya mashabiki na kufanya jumla ya tiketi zilizotolewa na serikali kufikia  tiketi 4000.

Wadau wengine wa soka walijitokeza kutoa ahadi za kununua tiketi kwaajili ya mashabiki ambao ni  mwenyekiti wa DRFA  Lameck Nyambaya (200), Rais wa klabu ya Young Africans Engineer Hersi Said (1500) Afisa mtendaji mkuu wa Azam Abdulkarim Amin (1000),Mwenyekiti wa klabu ya Simba SC Murtaza Mangungu (600),  Naibu Waziri wa kilimo Mheshimiwa Antony Mavunde (200), Mkuu wa mkoa wa Njombe Mheshimiwa Antony Mtaka (200).

Wengine ni Mbunge mstaafu  wa Jimbo la Kinondoni Idd Azzan (300), Abdallah Mwaipaya Mkuu wa wilaya ya Mwanga (100), Mmiliki wa Kitambaa cheupe Jessica kikumbi (300), Hashim Mbaga  Mwakilishi wa Swahili water (100), Lampard electronics (100), Bullet Force (100) na wengine wengi.

Jumla ya tiketi 10,500 zilipatikana katika mkutano huo, huku Ofisa habari wa TFF Clifford Ndimbo  pamoja na wasemaji wa klabu  mbalimbali ikiwemo Simba SC, Young Africans  pamoja na Azam FC wakihimiza  mashabiki kujitokeza kwa wingi kuiunga mkono timu ya taifa  ya Tanzania ili iweze kufanya vizuri katika michezo ya kimataifa.