Rais Samia aichangia Twiga Stars.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan ameichangia timu ya Taifa ya wanawake Twiga Stars kiasi cha shilingi milioni 15 katika tamasha la Orange Concert lililoandaliwa na Baraza la michezo la Taifa BMT wakishirikiana na taasisi ya Dada Hood katika ukumbi wa JNICC jijini Dar es Salaam.
Akiongea kwa njia ya simu na waziri wa Fedha Mh. Mwigulu Nchemba aliyekuwa mgeni rasmi wa tamasha hilo Rais Samia alisema “nimefuatilia tukio hili la uchangishwaji fedha kwa ajili ya Twiga Stars nikasema hii shughuli isinipite na niwapongeze kwa jambo kubwa mnalofanya. Kampuni nyingi zimechangia na mimi nimeona nitie mkono wangu hivyo nitachangia kama milioni 15, basi niwatakie kila la kheri na mkusanye fedha nyingi ili timu yetu iendelee kufanya vizuri kimataifa”.
Hii sio mara ya kwanza kwa Rais Samia kuziunga mkono timu za taifa za wanawake ikiwa ni juhudi za serikali ya awamu ya 6 katika kuliendeleza na kuliinua soka la wanawake hapa nchini. Kwa nyakati tofauti Mh. Rais aliweza kukutana na kuwapongeza Twiga Stars kwa kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania katika michuano mambalimbali ikiwemo COSAFA ambapo mwaka jana mwezi Octoba waliweza kutwaa ubingwa na kurejesha kombe nyumba na baadaye Mh. Rais aliwapatia zawadi ya viwanja katika mkoa wa Dodoma ikiwa ni namna mojawapo ya kuongeza hamasa na kutambua mchango wao katika sekta ya michezo.
Mbali na mchango wa Rais Samia, kampuni na taasisi nyingine pia ziliongezea nguvu ikiwemo Clouds Media Milioni 100, TPA Milioni 30, Taifa Gas Milioni 50, GSM Million 10, Tanga Cement Milioni 5, TRA Miliion 15, NSSF Million 5 pamoja na NBC ambao walitoa milioni 79, katika fedha hizo milioni 24 zitaelekezwa kwenye Bima za afya za wachezaji.
Tamasha la Orange concert liliandaliwa mahususi kwa ajili ya uzinduzi wa album ya muziki iliyopewa jina la “The Orange Album” pamoja na harambee ya kuchangia soka la wanawake kupitia Twiga Stars ikiwa ni namna moja wapo ya kuchagiza shamrashamra za kilele cha siku ya mwanamke Dunia inayofanyika tarehe 08/03 kila mwaka.