Rais Samia Aipongeza Serengeti Girls

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, aimwagia pongezi timu ya wanawake wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Girs) kwa kufanikiwa kufuzu kwenda kushiriki michuano ya Kombe la Dunia nchini India ifikapo Oktoba 11, 2022.

Mhe.Rais Samia alitoa pongezi hizo Julai 05, mwaka huu alipowaalika wachezaji hao na benchi la ufundi la timu hiyo kwenye hafla fupi ya kupata chakula cha mchana (Lunch) iliyofanyika Ikulu Dar es Salaam.

Akizungumzia kufurahishwa kwake na kufuzu kwa Serengeti Girls katika michuano ya Kombe la Dunia huko India, Rais alisema kuwa timu hiyo ya wasichana imeliheshimisha Taifa kwa kufuzu pamoja na kutoa mfungaji bora kwa Afrika Clara Luvanga, ambaye pia anashikilia nafasi ya pili ya ufungaji bora duniani kwenye michuano hiyo mikubwa.

Aidha, Rais Samia aliongeza kuwa hakuna mtu ambaye alitarajia kwamba Serengeti girls ingefikia mafanikio makubwa kwa kuweka historia ya kuipeperusha Bendera ya Tanzania katika soka Duniani.

“Watanzania hatukuamini kuwa watoto hawa wangeweza kufika huko lakini  wasichana hawa wameweza”. Alisema Rais Samia.

“Ninataarifa kuwa Tanzania haikushinda tu, bali imefanikiwa kutoa mfungaji bora Afrika na mfugaji bora wa pili Duniani; kwa hatua hiyo. niseme tu, Serengeti Girls imeliheshimisha Taifa letu, mmefanya jambo kubwa ambalo halijawahi kutokea nchini; hata wanaume hawajawahi kushiriki Kombe la Dunia lakini ninyi mmethubutu na mmeweza.”  Alisema Rais Samia

Mbali na hayo, Rais aliwatia moyo wachezaji, benchi la ufundi  pamoja na viongozi wote wanaosimamia soka hasa TFF akiahidi kuwa serikali anayoiongoza itaendelea kutoa ushirikiano wa hali na mali kuhakikisha timu hiyo na nyingine zinafanikiwa kufanya vizuri zaidi.  Rais aliimtia moyo mchezaji Clara Luvanga akimwambia kuwa anatambua ubora aliouonesha kwenye michuano hiyo kwa kumaliza akiwa na magoli 10 na kuwa mfungaji bora Afrika na wa pili Duniani kwamba aendeleze makali yake wala asisikilize maneno na usumbufu anaokumbana nao kutoka kwa baadhi ya wapinzani.

Alimpongeza pia Spika wa Bunge la Jumhuri ya Muungano wa Tanzania Tulia Akson kwa kutengua kanuni za Bunge na kuwaruhusu wachezaji hao kuingia Bungeni na kumpatia nafasi nahodha Noela Luhala kutoa neno la shukrani kwa niaba ya wachezaji wengine.

Tanzania imefanikiwa kufuzu kushiriki Kombe la Dunia kwa wasichana wa U17 baada ya kuzifurusha; Botswana 11-0, Burundi 4-1 na Cameroon 5-1. Kati ya timu tatu za Afrika zilizofuzu michuano hiyo Tanzania nayo imo; hivyo, haikufuzu kinyonge na kwamba inakwenda kushindana sio kushiriki. Timu nyingine zilizofuzu kutoka Afrika ni Morocco na Nigeria.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri mwenye dhamana ya michezo nchini Mohammed Mchengerwa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Hassan Abbas na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, Wallace Karia aliyeambatana na baadhi ya viongozi na wafanya kazi wa Shirikisho.