Rais Samia Akoleza Mzuka Stars, Aongeza Tiketi Elfu Tano na Aahidi Kila Bao 10Milioni
Rais wa Jumhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan ameongeza Idadi ya tiketi kutoka elfu mbili (2000) hadi tiketi Elfu Saba (7000) kwa ajili ya kuwagawia mashabiki wanaotaka kuiona Stars kwenye mchezo wao wa marudiano utakaopigwa Machi 28 kwa Mkapa.
Hatua hiyo imekuja baada ya Rais Samia kufurahishwa na matokeo ya ushindi wa 1-0 walioupata Stars ugenini walipokutana na Uganda, timu ambayo imekuwa ikitoa changamoto kila inapokutana na Taifa Stars.
Alikabidhi tiketi hizo kwa Rais Karia, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Saidi Yakubu alisema kuwa Mhe. Dkt. Samia ameridhishwa na kiwango cha Stars kilichooneshwa kwenye mchezo wa kwanza uliopigwa Machi 24, mwaka huu nchini Misri na kuibuka na ushindi wa bao 1-0, na kwamba sasa ameahidi kuongeza motisha zaidi kwa kununua kila goli litakalo patikana kwa kiasi cha fedha ya Kitanzania Milioni kumi(10,000,000).
Aidha, Katibu Mkuu Yakubu aliongeza kuwa baada ya Mhe. Rais Dkt Samia kuongeza tiketi 5,000 na kufikisha jumla ya tiketi 7,000 zinazofikia idadi ya elfu tisa (9000) pamoja za Waziri Mkuu; Wizara ya Utamaduni,Sanaa na Michezo imefanikiwa kujikusanya na kupata jumla ya tiketi elfu kumi na moja(11000) zinazofanya jumla ya tiketi 20,000 kutoka Serikalini ambazo tayari Wizara hiyo kupitia Katibu Mkuu Yakubu imekwisha kukabidhi kwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Wallace Karia kwa ajili ya kufanya utaratibu wa kuzigawa kwa mashabiki.
Akitoa neno la shukrani kwa Rais Samia kupitia kwa Viongozi wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, Rais Karia kwa niamba ya wanafamilia ya mpira nchini alimshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akieleza kuwa Dkt Samia amekuwa sehemu ya mafanikio ya Soka la Tanzania. Aliongeza kuwa hamasa anayoendelea kuitoa Rais Samia inaongeza Ari na Morali na Motisha ya wachezaji, lakini pia kuwavutia zaidi mashabiki ambao huenda baadhi yao wangelipata ugumu wa kununua tiketi ili kuenda kuiona timu yao ya Taifa; sasa wao kazi yao imebaki Moja ya kwenda uwanjani tu.
Aidha, Rais Karia aliweka rekodi sawa kuhusu ushindani wa Stars na The Crains kuwa katika michuano ya AFCON na CHALLENGE CUP, timu hizi zimakutana mara kadhaa lakini Tanzania imefanikiwa kupata matokeo mara mbili na sare moja huku akifafanua kuwa Uganda wamekuwa wakiisumbua zaidi Tanzania kwenye kusaka tiketi ya CHAN inayohusisha wachezaji wa ndani ambapo mwaka uliopita Uganda iliitoa Tanzania.
Katika hatua nyingine Rais Karia alitegua kitendaliwili kuhusu Uteuzi wa wachezaji wa “Taifa Stars” uliofanywa na Kocha Mkuu Adel Amrouche hivi karibuni, kuwa ulikuwa ni Uteuzi wake mwenyewe. Rais Karia Alieleza kuwa Uteuzi huo ulifanywa na Kocha Amrouche Mwenyewe; na kwamba kabla ya kukabidhiwa timu hiyo, tayari walikuwa na Mazungumzo naye ya muda Mrefu huku kocha huyo akipatiwa muda wa kuwafuatilia kwa ukaribu zaidi wachezaji wa Ligi Kuu pamoja na kupitia video mbalimbali za mechi za Stars ili kuweza kubaini uwezo wa wachezaji anaowahitaji.
Kuelekea mchezo huo wa Machi 28, 2023 kwa Mkapa, Kocha Mkuu amewajumuisha kwenye kikosi wachezaji wazoefu Shomari Kapombe na Mohammed Hussein kwa ajili ya kukiongezea nguvu kikosi chake kitakachoshuka kwenye mchezo huo wa marudiano na Uganda ambao ni Muhimu kwa Stars kushinda.