Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani FIFA Gianni Infantino ametuma salamu za pongezi kwa Klabu ya Simba kwa kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Infantino ametuma salamu hizo za pongezi kupitia kwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Wallace Karia.

Katika Salamu hizo Infantino amesema amefurahishwa kusikia Simba SC wamevikwa taji la Ubingwa wa Ligi Kuu 2018/2019 ikiwa ni mara ya pili mfululizo jambo ambalo ni la kupongezwa.

Amesema hayo ni majibu ya jitihada na juhudi na ameomba salamu hizo zifikishwe kwa Wachezaji,Kocha,Uongozi,Benchi la Ufundi,Madaktari pamoja na mashabiki na kuwataka kuendeleza uthubutu na hamasa.

Infantino kwa niaba ya Jamii ya Mpira Kimataifa ameishukuru Simba na TFF kwa kusaidia kusambaza ujumbe chanya wa Mpira wa Miguu ambao unajumuisha watu wote.

Akimalizia salamu zake kwa Rais wa TFF,Infantino amesema anatarajia watakutana kwenye Kongamano la 69 la FIFA litakalofanyika Paris.