Rais wa FIFA na Rais wa CAF Kuweka Jiwe la Msingi TFF Kigamboni
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani(FIFA) Gianni Infantino pamoja na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika CAF Patrice Motsepe wanataraji kuweka jiwe la msingi kituo cha ufundi cha TFF Kigamboni Oktoba 20, 2023.
Hayo yamesemwa na Rais wa TFF Wallace Karia baada ya kukamilika kwa ukaguzi uliofanywa na ugeni kutoka FIFA na CAF akiwemo Rais wa Shirikisho la Soka nchini Djibouti Souleiman Hassan Waberi Oktoba 19, 2023; ugeni huo ambao pia ni sehemu ya maandalizi ya mapokezi ya viongozi hao wakubwa wa soka.
Rais Karia alisema ugeni huo walioupata Oktoba 19, ni sehemu ya utangulizi wa jambo kubwa na la kihistoria linalotarajiwa kufanyika Oktoba 20 mwaka huu kituoni hapo, hivyo kilichofanyika ni kuwaonesha maeneo yote ya majengo pamoja na viwanja na kujadiliana namna nzuri ya uendeshaji wa tukio hilo kubwa na muhimu lililo mbele yao.
Hata hivyo, Marais wote hao wanatarajiwa kuwasili hapa nchini kesho asubuhi ambapo Rais wa CAF Patrice Motsepe ataanzia jijini Dodoma wakiungana na Rais Karia na viongozi wengine wa TFF kwaajili ya kuzungumza baadhi ya vitu na Mheshimiwa Rais Dr.Samia Suluhu Hassan na baadaye viongozi hao watarejea Dar es Salaam kuungana na Rais wa FIFA Gianni Infantino.
Ikumbukwe ugeni huo ni kufuatia uzinduzi wa mashindano ya African Football League (AFL) ambayo mchezo wa ufunguzi unatarajiwa kupigwa Oktoba 20, 2023 majira ya saa 12:00 jioni kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa ambapo timu ya Simba SC itawakaribisha Al hilaly ya nchini Misri.