Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mhe.Dkt.John Pombe Magufuli amekabidhi kiasi cha shilingi milioni 50 kwa timu ya Taifa ya Tanzania “Taifa Stars” kusaidia maandalizi ya timu hiyo kwa mchezo wake wa kufuzu Fainali za Africa 2019 dhidi ya Lesotho utakaochezwa Novemba 18,2018 huko Maseru nchini Lesotho.

Rais Magufuli ameitaka timu ya Taifa kufanya vizuri katika mchezo huo wa Kundi L utakaopigwa ugenini.

“Nimechoka na matokeo mabaya na Watanzania wamechoka lakini nina imani na ninyi na ninaomba mkafanye vizuri katika mchezo huo “ amesema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli ameupongeza uongozi wa TFF chini ya Rais wake Wallace Karia kwa kazi nzuri iliyofanya ndani ya kipindi cha mwaka mmoja toka uingie madarakani na kumtaka kuendelea na kasi hiyo.

Katika hatua nyingine Rais Magufuli amemtaka Rais wa TFF ndugu Karia kutohofia kuwaondoa viongozi wote ambao wanakwenda kinyume na maadili ya utawala bora ili kuendeleza imani kwa uongozi wake na mpira wa miguu kiujumla.

Akizungumza kwenye hafla hiyo Rais wa TFF Ndugu Karia amesema muelekeo wa TFF kwasasa ni mzuri na chini ya uongozi wake amekuwa akisimamia utawala bora.

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji beki Erasto Nyoni amesema wamepokea maneno ya Rais Magufuli kwa uzito mkubwa na watayafanyia kazi hawatamuangusha na nia ni kufanya vizuri.

Nyoni alimkabidhi jezi ya Taifa Stars Rais Magufuli ambaye alipoipokea akasema anakumbuka enzi zake akicheza mpira katika nafasi ya ushambuliaji kabla hajarudi kuwa mlinda mlango.

Kocha Mkuu Emmanuel Amunike amemshukuru mheshimiwa Rais Magufuli na kuahidi kufanya vizuri katika michezo inayofuata kwa kuanzia na mchezo dhidi ya Lesotho.

Rais Magufuli pia amekula chakula cha mchana pamoja na wachezaji wa Taifa Stars na viongozi wa TFF Ikulu.

Taifa Stars inayodhaminiwa na Bia ya Serengeti Premium Ipo nafasi ya pili kwenye kundi L ikiwa na alama 5 nyuma ya vinara Uganda wenye alama 10.