Want create site? Find Free WordPress Themes and plugins.

Rais Wallace Karia Azindua Rasmi Semina ya Uongozi na Utawala Bora Visiwani Zanzibar
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Wallace Karia, afungua semina ya Uongozi na Utawala Bora kwa wenyeviti wa vilabu vya Ligi Kuu Tanzania Bara na Visiwani Januari 23, 2021 katika kumbi za hoteli ya Verde Iliyopo Visiwani Zanzibar.
Akifungua semina hiyo Wallace Karia aliwashukuru wenyeviti wa vilabu mbalimbali shiriki wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Visiwani kwa kutenga muda wao na kukubali kuhudhuria semina hiyo; kwani hapo awali ilikuwa sio rahisi kupata mahudhurio mazuri kama hayo ya msimu huu na kwamba anamini kuwa kupitia wakufunzi watakao toa mafunzo hayo yataleta hamasa katika utendaji kazi kwa vilabu vyote Tanzania.
Aidha, alieleza kuwa lengo kubwa la (TFF) kwa kushirikiana na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) ni kuwajengea na kuwaongezea uwezo wenyeviti wa vilabu vya ligi kuu kuendesha mpira wa miguu kwa weledi na ufanisi mkubwa; kwani mchezo wa mpira wa miguu umebadilika kuanzia wachezaji hadi uendeshaji wake ndio maana wanasistiza vigezo vya leseni za vilabu kuzingatiwa na kufuatwa ili mchezo wa mpira wa miguu uweze kuendelea mbele zaidi nchini Tanzania kama ilivyo katika nchi za ulimwengu kwanza(Developed Countries).
Sambamba na hayo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Almas Kasongo alisema kuwa dhamira kubwa ya kuandaa semina kama hizo ni kutaka kusisitiza mambo muhimu yanayoendana na Uongozi na Utawala Bora ambayo yataleta tija katika ligi na mwisho kuuinua mpira wa miguu Tanzania pamoja na timu za taifa endapo itazingatiwa na kufuatwa kikamilifu. Aliongeza kwa kutoa mifano hai ya nchi zote ambazo zinasimamia vema vigezo vya utoaji wa leseni za vilabu kuwa soka lao liko juu na linakwenda mbio katika suala la ubora na viwango.
Naye Makamu wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Visiwani Zanzibar (ZFF), Salum Ubwa aliishukuru TFF kwa kusimama masuala ya soka la Tanzania ikiwa kama mzazi katika kuhakikisha kuwa yanakwenda vizuri huku ikiwa na dhamira ya kweli ya kuinua soka na kuboresha mikakati ambayo italeta faida kubwa kwenye mpira wa miguu nchini. Alisema TFF inaifanya kazi hiyo nchi nzima kuanzia Bara mpaka Visiwani; hivyo endapo vilabu husika vinavyoshiriki ligi nchini zitaamua kufuata maelekezo, hakika mpira wa Tanzania kwa ujumla utaenda mbali na ligi zitakuwa zenye ushindani ukilinganisha na nchi nyingine.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa semina hiyo, Selemani Mataso Mwenyekiti wa klabu ya Biashara United alitoa shukrani zake za dhati kwa nafasi adhimu na ya kipeke ya kushiriki katika mafunzo mbalimbali ambayo yamekuwa yakiendelea kutolewa kwenye semina hiyo na zile ambazo TFF imewahi kuzitoa. SMataso hakuishia hapo bali aliuomba uongozi mzima wa TFF kuendelea kutoa mafunzo kama hayo mara kwa mara; kwani yataleta tija katika maendeleo ya mpira miguu nchini Tanzania.

Did you find apk for android? You can find new Free Android Games and apps.