Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) Yaweka Wazi Ratiba ya Ligi Msimu wa 2020/2021Nchini
Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB), Almasi Kasongo ametangaza tarehe rasmi ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi kuu 2020/2021 na kutoa ratiba nzima ya ligi hiyo 17 Agosti 2020.
Hayo alisema katika Makao Makuu ya Ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) yaliyopo Karume, Karikoo-Dar es salaam.
Akitoa maelezo kuhusu Ligi hiyo, Kasongo alisema kuwa michezo ya kwanza ya ligi inatarajiwa kuanza tarehe 6 Septemba huku akiweka wazi kuwa mchezo wa kuzindua ligi yaani ule wa Nagao ya Jamii unatarajiwa kupigwa Jijini Arusha ambapo utazikutanisha kwa mara nyingine tena Simba SC na Namungo FC katika uwanja wa Shekh Amri Abedi, Arusha Tanzania.
Aidha Kasongo aliidhinisha rasmi kutolewa kwa ratiba ya msimu mpya wa 2020/2021 na kusema kuwa utakuwa na jumla ya timu 18 kama ambavyo kamati ya utendaji ilivyokwisha kupitisha.
Ofisa Kasongo alifafanua kuwa kupungua kwa idadi ya timu za ligi kuu msimu huu ni hatua mojawapo ya kuelekea kubaki na timu 16 huko mbeleni.
Hata hivyo, Kasongo alieleza kuwa mwisho wa msimu huu timu 4 zitashuka ili kukamilisha mchakato wa kubaki na timu 16.
Aliendelea kwa kusema, sambamba na hayo; katika ushiriki wa timu 18 kunatarajiwa kuwa na michezo 306 kutoka kuwa na michezo 380 na kuongeza kuwa kutakuwa na raundi 34 kwa maana michezo ya nyumbani na ugenini na kwamba wanatarajia kumaliza ligi tarehe 15 Mei, 2021.
Kasongo alibayanisha kuwa michezo ya ‘play off’ inatarajiwa kuchezwa siku nne tu baada ya ligi kuisha 19 Mei 2021 huku marudiano yakitarajiwa kuwa tarehe 23 Mei, 2021.
Vilevile, aliongeza kuwa ratiba hiyo imezingatia kalenda ya FIFA na CAF licha ya kuwa wao walikuwa hawajapata rasmi Kalenda za FIFA na CAF zinazoonesha ratiba za kalenda hizo na hivyo kudai kwamba wametumia uzoefu tu na kukadiria kama ilivyokuwa katika ratiba zao za awali, kulingana na utaratibu wa michuano husika.
Aliongeza kwa kusema kuwa endapo kutakuwa na mabadiliko yeyote ya kalenda, basi itegemewe kuwepo kwa mabadiliko kidogo kwenye ratiba hiyo pia.
Hata hivyo, Kasongo aliupongeza pia uongozi mzima wa ‘Azam Media’ kwa kuhakikisha ligi inaendelea kuoneshwa na kutoa fursa kwa wadau na mashabiki kushuhudia mubashara kabisa timu zao zikicheza michezo mbalimbali.
Alitoa ufafanuzi pia juu ya mpango wao mpya wa kutaka kuboresha baadhi ya viwanja ili kuwezesha mechi kuchezwa hata nyakati za usiku na kusema kuwa jambo hilo litaongeza chachu katika msimu mpya wa ligi.
Ofisa huyo wa Bodi ya Ligi Tanzania, alihitimisha kwa kutoa shukrani zake za dhati kwa serikali iliyo chini ya uongozi wa Dkt.John Pombe Magufuli hasa kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo; kwa ushirikiano inaowapatia TFF na TPLB kwa ujumla.
Wakati huohuo Kasongo aliwamwagia sifa waandishi wa habari wote pamoja na mashabiki wa mpira wa miguu nchini kwa kuonesha ushirikiano mkubwa katika msimu wa ligi uliopita na kuwaomba wadau wote kuendelea kuwa pamoja katika msimu mpya wa 2020/2021.