Raundi ya Pili TWPL Imemalizika

Michezo mitano ya ligi kuu Tanzania imepigwa kati ya Disemba 27 na 28, 2023 na kukamilisha raundi ya pili msimu huu, huku timu ya Simba Queens ikiwa kileleni mwa msimamo wa ligi kwa faida ya utofauti wa magoli.

Matokeo ya ushindi wa magoli 5-2 waliyoyapata Simba Queens kwenye mchezo wao wakiwa wenyeji na kuikaribisha  timu ya Baobab Queens ndio yaliyoifanya timu hiyo kukaa kileleni kwa tofauti ya magoli na timu nyingine 5 zinazo fuatia kwenye msimao.

Hata hivyo timu ya Yanga Princess ndio inayofuata nafasi ya pili kwa jumla ya alama 6 sawa na Simba Inayoongoza, JKT Queens na Allience Girls . Yanga Princess yenyewe imeshinda magoli 6-1 dhidi ya Amani Queens. Matokeo mengine yakiwa Bunda Queens 2-3 Allience Girls, Geita Gold Queens 0-1 JKT Queens na Fountain Gate Princess 3-2 Ceasiaa Queens.

Timu ya Ceasiaa Queens ndio inayoburuza mkia kwenye msimamo wa ligi ikiwa ndio timu iliyo fungwa magoli mengi zaidi baada ya kupoteza kwenye michezo yote miwili, licha ya kuwa pia hizo timu nyingine zinazofuatia zikiwa juu ya timu hiyo(nafasi ya 6-9) zote hazijaambulia kupata alama yoyote kwenye mechi zake.

Mpaka sasa ni timu mbili pekee ndizo zimecheza mchezo mmoja, hivyo ni kiporo cha mchezo mmoja pekee ambao ulibidi upigwe kwenye raundi ya kwanza kati ya Fountain Gate Princess na Amani Queens ndio utazifanya timu hizo kwenda sawa kwa kulingana kwa idadi ya mechi za kuchezwa.

Mbali na hayo ligi hiyo kubwa kwa wanawake hapa nchini TWPL inatarajiwa kuendelea mapema mwakani Januari 2, 2024 kwa mechi zitakazo pigwa nje ya Dar es Salaam, kabla ya mchezo mkubwa utakaopigwa Januari 3, 2024 kati ya miamba ya ligi hiyo (Watani wa jadi) Simba Queens dhidi ya Yanga Princess.