Raundi ya Tano TWPL Yazidi Kupamba Moto

Ligi kuu ya wanawake Tanzania TWPL 2023/2024, joto limezidi kupanda baada ya mechi za raundi ya tano kumalizika kwa matokeo yanayodhihirisha ubora na kila timu kukiimarisha katika kila maeneo hasa nna ya kuwakabili wapinzani kwa mbinu tofauti.

Mechi hizo tano za raundi ya tano zimechezwa kwa siku mbili Januari 15 na 16, 2023 huku kila timu ikidhihirisha namna walivyoipanga mipango mikakati ya kuendea  michezo yao huku kila mmoja akionekana kutafuta nafasi nzuri na salama zaidi kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Matokeo ya mechi ya kwanza raundi ya tano yalimalizika kwa timu ya JKT Queens kubakiza alama tatu nyumbani kwa ushindi wa magoli 5-0 dhidi ya Allience Girls mchezo uliopigwa uwanja wa Azam Complex Chamazi Januari 15,2024.

Hata hivyo kwenye raundi hiyo ni michezo miwili iliyofanikiwa kumalizika kwa matokeo ya idadi sawa ya mabao matano. Wakati JKT Queens ikiifunga  Allience Girls 5-0 mchezo mwingine uliomalizika kwa matokeo sawa ni ule uliomalizika kwa Amani Queens 2-3 Simba Queens.

Matokeo mengine ni; Geita Gold Queens 0-2 Bunda Queens, Baobab Queens 2-2 Fountain Gate Princess na Yanga Princess 0-1 Ceasiaa Queens. Matokeo ambayo timu za JKT Queens, Simba Queens na Yanga Princess zikiwa nafasi tatu za juu.

Geita Gold Queens ikiwa inaburuza mkia bila alama yoyote baada ya kupoteza michezo yake yote mitano, ikifuatiwa na Amani Queens kwenye nafasi ya 9 yenye alama tatu pekee na Baobab Queens ikiwa na jumla ya alama 4 zikiwa ndio timu tatu za mwisho kwenye msimamo wa ligi kuu ya wanawake msimu huu.